• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
TAHARIRI: Ni bora michezo kurejea shuleni

TAHARIRI: Ni bora michezo kurejea shuleni

KITENGO CHA UHARIRI

HATUA ya Muungano wa Michezo katika Shule za Upili Nchini (KESSSA) kupendekeza michezo irejelewe ni ya kusifiwa.

Mnamo Machi 2020 michezo katika taasisi zote za elimu nchini ilisitishwa mara moja baada ya kisa cha kwanza cha homa ya corona kuripotiwa.

Hali hii imesalia vivyo hivyo hata baada ya shule kufunguliwa mwishoni mwa mwaka jana hadi leo.

Kwa hakika, baadhi ya mashindano kama vile mpira wa vikapu, magongo (hoki), raga na handiboli yalikuwa yamepiga hatua kubwa na kufikia viwango vya juu.

Baada ya shule na vyuo kufungwa tena mwezi wa Machi na kufunguliwa mwezi huu, wadau wametambua haja ya michezo kufunguliwa ili kutekelezwa sambamba na masomo shuleni na vyuoni.

Akitangaza mabadiliko haya mnamo Alhamisi, Mwenyekiti wa kitaifa wa KESSSA Bw Peter Oraro, alisema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa michezo kurejelewa Julai. Hii ni baada ya maafisa wa Wizara ya Elimu na wale wa KESSSA kufikia uamuzi kwamba kulikuwa na haja kubwa michezo ifufuliwe katika taasisi za elimu haraka iwezekanavyo. Waliwasilisha ratiba ya shughuli hizo kwa waziri wa Elimu Profesa George Magoha ili aweze kuidhinisha.

Mashindano yatakayorejelewa ni pamoja na yale ya uigizaji (drama), muziki, riadha na mpira. Yanapaniwa kutekelezwa katika shule zote, vyuo vyote na taasisi zote kwa jumla nchini.

Kwa hakika, kama wadau hawa walivyodokeza, kuna talanta nyingi ambazo zimepuuzwa na huenda zikaoza na kuozeana zikikosa kukuzwa wakati ufaao. Kulaza vipaji kwa miaka miwili bila kuvinoa ni hatari kwa vinaweza kutokomea kabisa. Isisahaulike wanafunzi wengi katika shule za upili wako kwenye kilele cha kutambua na kukuza vipaji vyao. Katika enzi hizo za leo, si siri kwamba michezo imegeuka kuwa asili ya ajira na kwa sababu hii ni lazima ithaminiwe kikamilifu.

Kwa matumaini kwamba mipango hii itafanikishwa, ni bora washiriki wa mashindano wazingatie kikamilifu maagizo na masharti mapya ya Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya gonjwa hili hatari la Covid na hasa ile aina mpya kutoka India ambayo imefika humu nchini.

Kanuni hizi zikifuatwa bila shaka zitaleta ukamilifu katika ukuaji wa watoto wetu kisaikolojia masomoni. Ufunzaji utarahisishwa kwani nidhamu za wanafunzi zitaimarishwa kupitia michezo bila kutaja manufaa ya kiafya, kimwili na kiakili.

You can share this post!

KAMAU: Serikali isiwasaliti wanafunzi kwa kuwanyima mikopo

Corona imeua wengi zaidi kinyume na taarifa – WHO