• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
DINI: Muda hauna rafiki, ukipotea haufufuki, utumie vizuri kujiendeleza kimaisha

DINI: Muda hauna rafiki, ukipotea haufufuki, utumie vizuri kujiendeleza kimaisha

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

SAUTI ya muda inasema, ‘muda sio rafiki.’

Muda sio kwamba unakimbia tu bali una mabawa, unapaa. Hivyo usiupoteze katika mambo ambayo hayakusaidii kutimiza malengo yako.

“Sauti ya muda inamlilia binadamu, ‘piga hatua mbele.’ Muda ni kwa ajili ya maendeleo yake na uboreshaji kwa ajili ya thamani yake kubwa, furaha yake kubwa, kwa ajili ya maisha yake bora,” alisema Charles Dickens.

Tumia muda kuboresha mazuri yawe mazuri zaidi. Mtume Paulo anatukumbusha, “Ndugu, nasema hivi: muda ni mfupi” (1 Wakorintho 7:29).

Kumbuka ukiua muda, muda haufufuki. Kumbuka ukiuzika muda, muda haufufuki. “Hazina zote za dunia haziwezi zikarudisha kitambo kimoja kilichopotea” (Methali ya Kifaransa). Hakuna kiasi kikubwa chochote cha dola ambacho kinaweza kurudisha dakika iliyopotea. Jana haifufuki. Juzi haifufuki. Siku chache zilizopita hazifufuki. Mwaka jana haufufuki. “Anayeua muda anajiua” (Fred Beck).

Muda unaouua ungeutumia kufanya kazi inayolipa na kuwa na makazi mazuri, angeutumia kupata lishe bora, angeutumia kupata pesa ya kulipia huduma hospitalini iwapo ni mgonjwa.

Usiwe mtumwa wa kesho. Waziri wa afya wa Uingereza bwana Aneurin Bevan alipotoka kuitembelea Urusi aliombwa kuelezea jambo kubwa alilolingundua Urusi. Alijibu, “Jambo kubwa nililoligundua ni kuwa wakati hapa Uingereza tunakuwa watumwa wa muda uliopita, Urusi ni watumwa wa wakati ujao.” Hayo yalikuwa maoni yake. Yawe kweli yasiwe kweli tunajifunza kuwa kuna uwezekano wa kuwa mtumwa wa wakati uliopita au mtumwa wa wakati ujao.

Kwa mtumwa wa kesho, kila kitu kitafanyika kesho. Kwa mtumwa wa kesho na siku fulani, kesho ni siku atafanya mambo. Kwa mtumwa wa kesho liwezekanalo leo lifanyike kesho. Kwa mtumwa wa kesho kuhaihirisha ni kawaida. “Ni tendo kubwa kutokuacha jambo lolote kwa ajili ya kesho” (Baltasar Gracian).

Usiwe mtumwa wa jana. Mtumwa wa jana anaifikiria jana muda wote. Utamsikia mtu anasema, zamani nilisali sana kanisani. Sasa imekuwaje? Tulipokuwa vijana vitu vilinunuliwa kwa bei rahisi. Si vizuri kukaa umetazama wakati uliopita. Ishi sasa. Wakati uliopita ukusaidie kuboresha wakati wa sasa. Kwa mtumwa wa jana, jana inaonekana ni siku kubwa sana. “Kama ulilolifanya jana linaonekana ni kubwa, leo haujafanya lolote” (Lou Heltz).

Jina la Mungu ni “MIMI NIKO AMBAYE NIKO” (Kutoka 3: 13). Hili ndilo jina ambalo Mungu alimtajia Musa.

Mungu si mtumwa wa jana na si mtumwa wa kesho. Hakusema mimi ni Atakayekuwepo. Hakusema, mimi niliyekuwepo, alisema, MIMI NIKO AMBAYE NIKO. Yeye ni wa milele. Si mtumwa wa jana ndiyo maana anasamehe kwa yeyote anayetubu.

“Kumbatia upekee wako. Muda ni mfupi sana kuishi maisha ya mwingine kwanza,” alisema Kobi Yamada. Wewe kama wewe una ndoto. Wewe kama wewe una mipango. Wewe kama wewe una kitu unachokitaka. Kuna mambo yanayokutofautisha na wengine. Usipokuwa makini unaweza kutekeleza ndoto za wengine na kusahau ndoto zako maisha yako yote.

“Niambie unavyotumia muda wako wa ziada na nitakwambia utakapokuwa miaka kumi ijayo,” alisema Napoleon Hill.

Matunda ya kesho yamo kwenye mbegu za leo. Kama haupandi mbegu leo, miaka kumi ijayo utakuwa na maisha ya shida.

Usitumie muda wako wa ziada kufanya mambo yasiyo na tija. Tumia muda wako wa ziada kuzalisha mawazo na kupanda mbegu.

Wakati wa muda wa ziada unaweza kulima bustani, kupanda miti, kufanya utafiti, kucheza michezo, kusoma vitabu, kujifunza, kumaliza viporo vya kazi, kutaja machache. Ukweli unabaki liwezekanalo leo lisingoje kesho, muda sio rafiki.

You can share this post!

MALENGA WA WIKI: Mwangi Wanjiru ni miongoni mwa vijana...

Bingwa wa ukaidi