Chupi za kimada zanaswa mvunguni

Na JOHN MUTUKU SAMUEL

UMOJA ONE, Nairobi

MIPANGO ya polo wa hapa kuhama nyumba ilivurugika mkewe alipopata chupi ambazo kimada wa mumewe alificha chini ya kitanda.

Kugunduliwa kwa ngotha hizo kulisababisha mzozo uliotishia kuvunja ndoa yake ya miaka miwili.

Polo alikuwa na mipango kadhaa ya kando na hakuona aibu kuwaleta wanawake katika nyumba mkewe akisafiri. Ili majirani wasigundue tabia yake alikuwa akiwaleta wanawake hao usiku na kuwasindikiza alfajiri.

Miongoni mwa mademu hao, kuna mmoja aliyedhani alifika kwa polo na hakukuwa na yeyote wa kumng’oa pale. Alihakikisha kila alipomzuru polo, alificha chupi chini ya kitanda. Nia yake ilikuwa mke wa polo agundue chupi hizo, ili naye apate nafasi ya kummiliki polo.

Siku ya tukio, polo aliwaita vibarua kumsaidia kupangua vitu. Walipofungua mbao za kitanda, kule mvunguni walipata chupi sita zilizotiwa kwenye mfuko. Walimpokeza mkewe na kuona haya kushika nguo hizo. Hapo ndipo yowe lilipomtoka mkewe.

“Una nini jamani?” wanaume hao waliuliza. Dakika chache baadaye polo aliingia na kushangaa kumpata mkewe chozi kifua tele.

“Wewe ni ndumakuwili! Hizi nguo ni za nani?” demu alimkabili mumewe.

Tafadhali mke wangu, usikasirike. Nitakueleza,” polo alimbembeleza.

“Unieleze nini? Hizi ni chupi za mwanamke mwingine,” demu alisisitiza.

“Mbona uko hivyo? Mbona wanikosea heshima ukitembea nje ya ndoa? Ni kipi ukosacho kwangu ili ukatembee na wanawake wengine?Siwezi kuishi na mkware, nina heshima zangu. Chumba nilichoacha kwetu kingalipo,” mke alipakia nguo na kutoka kwa ghadhabu.

“Wanaume wengine ni wanyama,” mke alisema hayo na kuondoka bila kutazama nyuma.

Hata hivyo, haijulikani iwapo suluhu ilipatikana baadaye.