• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
JAMVI: Mwamko mpya Pwani 2022

JAMVI: Mwamko mpya Pwani 2022

Na WAANDISHI WETU

UKANDA wa Pwani huenda ukapata magavana wa kwanza wa kike katika uchaguzi mkuu ujao, iwapo wanasiasa walioonyesha maazimio kufikia sasa hawatalegeza kamba.

Kaunti tatu za Pwani tayari zimevutia wanasiasa wa kike walio na ari ya kuondoa dhana kuwa wadhifa huo unastahili kuwa wa wanaume pekee.

Wanasiasa hao ni mbunge wa Malindi Aisha Jumwa anayemezea mate ugavana wa Kaunti ya Kilifi, Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani anayetaka kupanda ngazi uongozini katika kaunti hiyo kisha yupo mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko anayemezea mate ugavana wa Mombasa naye mtaalamu wa haki za kijamii, Bi Umra Omar anaangazia wadhifa huo katika Kauntui ya Lamu.

Wanne hawa wameonyesha nia ya kutaka kuwarithi magavana Amason Kingi, Salim Mvurya, Hassan Joho na Fahim Twaha mtawalia.

Kaunti nyingine za Pwani ni Taita Taveta na Tana River ambapo kufikia sasa hakuna mwanamke aliyejitokeza wazi akiazimia kuwania ugavana 2022.

Mnamo wikendi, Bi Jumwa aliendelea kusisitiza kuhusu azimio lake la kutaka kuwa mrithi wa Bw Kingi.

Mbunge huyo aliye mtetezi sugu wa Naibu Rais William Ruto, alisema hayo alipohudhuria mazishi eneo la Rabai.

Baadaye kupitia kwa mtandao wa Twitter, alitangaza kwamba ‘Kilifi itaongozwa na mwanamke 2022’.

Azimio lake limepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanawake wa kaunti hiyo ambao tayari wameanza kumpigia debe.

Aliyekuwa Seneta Maalum wa Jubilee, Bi Emma Mbura alisema umefika wakati kwa wakazi wa Kilifi kuwa na kiongozi mwanamke ambaye ataendeleza ajenda ya kupiga vita umaskini.

“Sisi wanawake ndio tunaelewa shida tunazozipitia shuleni, hospitalini na shida ya maji ambapo inawalazimu kina mama kutembea mwendo mrefu ili kupata huduma hizo,” akasema.

Aliongeza kuwa wanaume katika Kaunti ya Kilifi wamekuwa wakieneza chuki na siasa za kuwagawanya wanawake ili kutoa twasira kuwa wanawake ni adui wao wenyewe.

“Mara hii akina mama tutazunguka na kukesha hadi tuhakikishe kuwa kiti cha ugavana tunampa mwenzetu. Tunataka kuona uongozi wa mwanamke utatusaidia vipi,” akasema Bi Mbura.

Katika Kaunti ya Kwale, hali isiyo ya kawaida imeibuka ambapo gavana wa sasa amejitokeza wazi kumpigia debe naibu wake amrithi. Kwa kawaida humu nchini, uhusiano kati ya magavana na manaibu wao katika kaunti nyingi huwa si mzuri.

Lakini Gavana Mvurya amekuwa akimpigia debe Bi Achani, akiamini kwamba ndiye kiongozi bora aliye na uwezo wa kuendeleza mbele miradi ya maendeleo iliyokuwa imeanzishwa na utawala wake.

Katika hafla ya majuzi zaidi, gavana huyo alimsifu naibu wake kama anayestahili kumrithi. Alitoa mfano wa Tanzania ambapo Rais Samia Suluhu alipokezwa mamlaka kikatiba baada ya kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli.

Akizungumza katika mazishi ya Askofu Morris Mwarandu mwezi uliopita, gavana huyo alisema ni Bi Achani pekee atakayeweza kuendeleza mafanikio ambayo kaunti hiyo imeshuhudia tangu 2013.

“Ni vile hapa ni mazishini sitaongea zaidi. Lakini Askofu aliniambia ‘muda wako unaisha hivyo ututayarishie siku za usoni’. Naibu gavana ametayarishwa. Mnaona Tanzania hakujawa na msukosuko. Katika taasisi ni lazima watu watayarishwe,” akasema.

Kwa upande wake, Bi Mboko ambaye ni mwandani wa Gavana Joho, amekimezea mate kiti hicho kwa muda sasa ingawa kufikia sasa hajajitokeza kimasomaso.

Azimio lake lilikuwa tayari limepokea uungwaji mkono kutoka kwa wanawake ndani na nje ya kaunti hiyo hasa kupitia kwa vuguvugu la wanawake wanaounga mkono handisheki, la Embrace.

Katika Kaunti ya Lamu, Bi Umra Omar aliambia Taifa Jumapili katika mahojiano ya awali kwamba hataruhusu tamaduni zinazodhalilisha wanawake eneo hilo kuzima azimio lake la kutaka kuwa gavana.

Bi Omar ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijamii, ndiye mwanzilishi wa shirika la Safari Doctors ambalo limepokea tuzo tele kimataifa kwa kujitolea kufikisha huduma za matibabu kwa umma kupitia njia ya barabarani, angani na baharini.

“Mimi ni mwanamke wa Kibajuni lakini hilo halitanizuia kupigania kile ninachoamini ni haki. Naamini kiongozi mwema hafai kuogopa visiki vilivyo mbele yake. Kwa hivyo nahimiza wanawake hapa wasiruhusu ubaguzi dhidi ya wanawake”, akasema.

Mwanaharakati wa Lamu, Bi Raya Famau, alisifu uamuzi wa Bi Omar kuwania ugavana katika kaunti hiyo.

Bi Famau alisema hatua hiyo ni bora kwa wanawake wa Lamu ambao kwa miaka mingi wamekandamizwa na mila na desturi za kibaguzi ambazo hupendelea wanaume.

“Ubaguzi dhidi ya wanawake unatokana na ubinafsi. Tunaweza kuinuka dhidi ya kila aina ya ubaguzi tunaorushiwa na kuongoza si kaunti hii pekee bali nchi nzima. Hakuna tatizo lolote katika kuwa na gavana wa kike, mbunge, seneta au hata kiongozi wa taifa,” akasema Bi Famau.

Tangu ugatuzi ulipoanza kutekelezwa mwaka wa 2013, Kenya imekuwa na magavana watatu pekee wa kike ambao ni Anne Waiguru (Kirinyaga), Charity Ngilu (Kitui) na Joyce Laboso (Bomet). Bi Laboso alifariki katika mwaka wa 2019 baada ya kuugua saratani.

Ripoti za Charles Lwanga, Maureen Ongala, Valentine Obara na Kalume Kazungu

You can share this post!

Real Madrid wakamilisha kampeni za msimu huu wa 2020-21...

Kisumu ingali juu kwa visa vipya vya corona