• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Shughuli ya utoaji chanjo ya polio yazinduliwa Kiambu

Shughuli ya utoaji chanjo ya polio yazinduliwa Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

SHUGHULI ya utoaji chanjo ya polio imezinduliwa Kiambu.

Waziri wa Afya wa Kaunti hiyo Dkt Joseph Murega, alisema shughuli hiyo iling’oa nanga Mei 22 na inatarajiwa kuendelea hadi Mei 26, 2021.

Alieleza tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha ya kwamba wauguzi wanazuru mitaa hadi vijijini kuona ya kwamba watoto chini ya miaka mitano wanapokea chanjo hiyo.

“Tunawahimiza wananchi hasa wazazi walio na watoto chini ya umri wa miaka mitano kushirikiana na wauguzi hao wa afya ili mpango wote uweze kufana,” alifafanua Dkt Murega.

Aidha, alieleza kuwa wauguzi hao watajitambulisha kwa wazazi walio na watoto wadogo ili kusiwe na tashwishi yoyote kuhusu mpango huo.

Alisema Wizara ya Afya ya hadhi ya kitaifa inataka kuona ya kwamba inaangamiza ugonjwa wa polio kwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano.

Wazazi wote wenye watoto wamehimizwa wakubali watoto wao wapewe chanjo ili kuzuia wao kuambukizwa na polio.

Dkt Murega alieleza kuwa kuna chanjo za kutosha na kwa hivyo wizara ya Afya itafanya juhudi kuona ya kwamba inatoa chanjo kwa watoto wengi.

Shughuli ya kutoa chanjo hiyo ilizinduliwa Ijumaa ambapo serikali ya kitaifa ikishirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto (UNICEF).

Serikali imeamua kutoa chanjo kwa sababu hivi majuzi aina ya polio iligunduliwa katika majitaka jijini Mombasa, ukanda wa Pwani.

You can share this post!

Haaland abadilishana jezi na refa anayestaafu baada ya...

Maelfu walazimika kuondoka katika makazi yao kufuatia...