• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Fumbo kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Bashir

Fumbo kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Bashir

NA MARY WAMBUI

MASWALI yanaendelea kuibuka iwapo mfanyabiashara Mohamud Bashir aliyeuawa katika hali ya kutatanisha, alikuwa akisakwa na maafisa wa usalama au wahalifu sugu waliotaka kumuua kwa sababu ambazo bado ni fumbo.

Mwili wa Bashir ulitambuliwa na jamaa zake katika hospitali ya Kerugoya baada ya kutekwa nyara mtaani Lavington, Nairobi mnamo Mei 16. Mwili wake ulipatikana ukielea ndani ya mto Nyamindi Mei 16 kabla ya kupelekwa hospitalini humo kama mtu ambaye hakutambulika.

Kwa mujibu wa polisi eneo la Kirinyaga, mwili wake ulipatikana ukiwa uchi pamoja na majeraha mabaya usoni yalitokana na kupigwa risasi mbili. Mwili huo ulipatikana kabla ya mawikili wa mfanyabiashara huyo kuwasilisha kesi mahakamani kuilazimisha idara ya usalama kufichua iwapo alikuwa akizuiliwa na maafisa wa serikali au la.

“Tulikuwa tumejiandaa kuwasilisha kesi hiyo mahakamani Ijumaa lakini korti ikafunga mapema. Kinachoshangaza ni kwamba, mnamo Jumamosi, tulipokea habari mbaya kuhusu kifo chake,” akasema wakili wa Bw Bashir Charles Madowo.

Maafisa wa usalama nchini hata hivyo, wamesalia kimya na haifahamiki iwapo mfanyabiashara huyo alikuwa akifuatiliwa kwa tuhuma za kushiriki ugaidi au kwa sababu za uhalifu.

Kamanda wa polisi Nairobi Augustine Nthumbi alieleza Taifa Leo kwamba, uchunguzi unaendelea kuhusu mauaji hayo lakini kufikia jana, hawakuwa wamepiga hatua yoyote.

Mawakili wake walisema uchunguzi wa post mortem kwenye mwili wake unatarajiwa kufanyika leo kabla hajafanyiwa mazishi kulingana na itikadi ya dini ya Kiislamu.

Marehemu alikuwa mfanyabiashara mtajika ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya ujenzi ya Infinity. Alikuwa akimiliki kampuni hiyo pamoja na wafanyabiashara wengine Kenya na ilikuwa ikiendeleza biashara Nairobi, Mogadishu na Milki ya Kiarabu.

Kati ya miradi aliyokuwa akiendeleza ni ujenzi wa kituo cha kisasa cha kibiashara cha Uhuru kwa kima cha Sh600 milioni jijini Kisumu. Pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, walikagua mradi huo mnamo Oktoba 22 mwaka jana. Pia kampuni yake ilijenga kasri la Rais wa Somalia.

You can share this post!

NANI ATALIPA HAWA WAZITO?

Utawala wa Sossion katika KNUT hatarini