• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
Wavuvi kuishtaki serikali upya kuhusu fidia

Wavuvi kuishtaki serikali upya kuhusu fidia

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wavuvi 4,000 walioathiriwa na mradi wa Bandari ya Lamu wanajiandaa kuelekea mahakamani wiki hii kuishtaki upya serikali kuhusu fidia.

Wamelalamika kuwa serikali imekosa kutimiza ahadi yake ya kuwalipa fidia ya Sh 1.76 bilioni.

Mwezi uliopita, serikali ya kitaifa ilikuwa imeahidi kwamba ingewalipa wavuvi hao fedha zao kama ilivyokuwa imeamrishwa na Mahakama Kuu mjini Malindi mnamo Mei, 2018.

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) na ile ya kusimamia mradi mzima wa bandari na uchukuzi kati ya Lamu inayounganisha Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia (Lapsset) ilikuwa imeahidi kuwalipa wavuvi hao kufikia katikati mwa Mei.

Mpango ulikuwa kwamba wavuvi wapokee fidia zao kabla Rais Uhuru Kenyatta kufungua rasmi Bandari ya Lamu mnamo Mei 20.

Aidha ahadi hiyo haijatimizwa hadi sasa licha ya Rais Kenyatta kuongoza hafla ya ufunguzi wa Bandari ya Lamu Alhamisi juma lililopita.

Akizungumza na Taifa Jumapili, Mwenyekiti wa Wavuvi, Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Somo alisema tayari wanajiandaa kupitia usaidizi wa mawakili wao ili kuishtaki serikali kwa kukiuka ahadi iliyoweka ya kuwalipa wavuvi.

Bw Somo alisema inasikitisha kuwa licha ya wavuvi kukubaliana na serikali kwamba wangejadiliana ili kutatua mzozo huo nje ya mahakama, serikali hiyo hiyo imewageuka wavuvi na kuwaacha bila namna.

“Waliturai kuondoa kesi mahakamani na tukakubaliana kwamba sote tungelipwa fidia yetu ya Sh 1.76 bilioni kabla ya bandari ya Lamu kufunguliwa mwezi huu. Kwa nini serikali ikaenda kinyume na matakwa hayo na kufungua bandari bila hata kutufidia sisi wavuvi?” akauliza Bw Somo.

Alizidi kusema kimya cha serikali kuhusu suala hilo ni ishara kuwa wavuvi wamesahaulika. “Tunajadiliana na mawakili wetu na mashirika mengine. Tutafika mahakamani juma hili ili kudai haki yetu. Tumechoka kudhulumiwa,” akasema.

Mmoja wa wavuvi walioathiriwa, Bw Mbwana Shee alimwomba Rais Kenyatta kuingilia kati na kuhakikisha wavuvi wa Lamu wanafidiwa ili kujiendeleza maishani.

Wavuvi hao wanadai fidia baada ya sehemu walizotegemea kwa uvuvi kuharibiwa na uchimbaji uliotekelezwa eneo la Kililana ambapo bandari ilijengwa.

Naye Bw Mohamed Athman ambaye ni Mwenyekiti wa Muungano wa Kutetea Haki za Wakazi wa Lamu wa Save Lamu, aliahidi ushirikiano katika kuhakikisha wavuvi wa Lamu wanapata fidia zao.

“Njia zao za uvuvi zimefungwa tangu uchimbaji baharini utekelezwe katika ujenzi wa bandari. Kwa nini serikali inaona ugumu kuwalipa hawa wavuvi maskini? Lazima haki itendeke,” akasema Bw Athman.

You can share this post!

Utawala wa Sossion katika KNUT hatarini

Wakazi Vihiga wakusanya saini kuvunja serikali ya kaunti