• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Wakazi Vihiga wakusanya saini kuvunja serikali ya kaunti

Wakazi Vihiga wakusanya saini kuvunja serikali ya kaunti

Na Derick Luvega

MPANGO wa raia ambao huenda ukasababisha Kaunti ya Vihiga kuvunjiliwa mbali ulizinduliwa jana katika hatua ambayo haikutarajiwa.

Hii ni kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya afisi pamoja na ufujaji wa fedha za umma miongoni mwa maafisa wa kaunti hiyo.

Wakazi waliokasirishwa na jinsi kaunti hiyo inavyoendeshwa, walianzisha shughuli ya kukusanya saini ili kuwasilisha malalamishi kwa Rais Uhuru Kenyatta wakimtaka kuvunja serikali ya kaunti hiyo.

Mpango huo kwa jina Hatua ya Raia wa Kaunti ya Vihiga, unaongozwa na Bw Joseph Simekha, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na aliyekuwa Katibu wa Kaunti, Bw Francis Ominde.

Wawili hao walisema mchakato huo wa wiki moja wa kukusanya sahihi kuhusu azma yao, unajikita katika misingi sita dhidi ya utawala wa eneo hilo.

Wakiorodhesha misingi hiyo sita, Bw Simekha na Bw Ominde walioambatana na baadhi ya wakazi, walisema wanatumia Kipengele 192(1) (b) cha Katiba kama suluhisho la mwisho la kukomboa Kaunti hiyo.

Kaunti ya Vihiga ina wapiga kura 280,000 waliosajiliwa na sheria inahitaji walalamishi kukusanya saini kutoka kwa asilimia 10 ya wapiga kura wote waliosajiliwa.

Bw Simekha alisema wameweka msingi wao na wamejiandaa vyema ili kuhakikisha wanapata saini 30,000, ambazo ni 2,000 zaidi ya idadi inayohitajika, kufikia mwishoni mwa wiki.

Kwa sasa, Gavana Ottichilo anakabiliana na kesi nyingine katika Mahakama Kuu ya Kisumu inayotaka atangazwe kama mtu asiyefaa kushikilia afisi ya umma.

Serikali yake, hata hivyo, ilipuuzilia mbali mpango huo wa kuivunjilia mbali ikisema ni njama za kutatiza ajenda ya bosi wa kaunti hiyo kuhusu maendeleo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari katika Afisi ya Gavana, Victor Wetende, usimamizi wa kaunti hiyo ulisema kesi hiyo haiwezi kwenda popote kwa kuwa waanzilishi wake ni watu wawili pekee wakilinganishwa na maelfu ya wakazi wanaoishi humo.

Gavana huyo aliwahimiza wakazi kuwapuuza waanzislishi wa kesi hiyo wanaolenga kukatiza uongozi wake.

Iwapo mpango huo utafanikiwa, kesi hiyo huenda ikamrejesha nyumbani Gavana Ottichilo, mawaziri wake na madiwani 38 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Hii imefanikisha kesi dhidi ya serikali ya kaunti,” alisema Bw Simekha.

You can share this post!

Wavuvi kuishtaki serikali upya kuhusu fidia

Mswada wa mbunge kuinua sekta ya sukari