Raila alakiwa kishujaa tayari kwa Madaraka

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Kisumu jana walipuuzilia mbali masharti ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) na kukusanyika kwa wingi katika vituo mbalimbali ambako kinara wa chama cha ODM Raila Odinga alisimama kuwahutubia.

Bw Odinga aliyetangulia Kisumu kukagua miradi ya maendeleo itakayozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta, alisimama katika Kituo Kikuu cha Mabasi, Kondele na Mamboleo ambako alifafanua umuhimu wa miradi hiyo ya maendeleo kwa watu wa Kisumu, kabla ya Sikukuu ya Madaraka wiki ijayo.

Japokuwa Kisumu imeshuhudia ongezeko la visa vya corona katika siku chache zilizopita, ziara ya Bw Odinga ya kukutana na watu ilivutia umati mkubwa kila alikosimama.

Kiongozi huyo wa ODM aliwaambia wakazi hao kuwa hata yeye mwenyewe alikuwa karibu akate tamaa alipoambukizwa ugonjwa wa Covid-19, lakini akapambana nao na sasa yuko imara.

“Siku nyingine shetani alikuja kwangu kwa jina la Covid-19 lakini nilipambana naye na nikamshinda. Sasa mnaweza kuona niko imara, mwenye furaha na afya. Nyinyi ndio watu wa kwanza ambao nimewatembelea tangu nipone, kwa sababu Kisumu ni nyumbani,” akasema.

Mipango ya mji wa Kisumu kuwa mwenyeji wa sherehe za Madaraka Dei mwaka huu inaendelea licha ya tishio la ugonjwa wa Covid-19 katika eneo hilo la Ziwa. Sherehe hizo zitafanywa katika uwanja wa michezo wa Jomo Kenyatta mjini humo, ambapo ni watu 3,000 pekee watakaoruhusiwa kuhudhuria.

Uwanja huo una uwezo wa kubeba mashabiki 35,000.

Katibu katika wizara ya Mambo ya Ndani, Dkt Karanja Kibicho, wiki jana alitembelea uwanja huo kukagua maandalizi ya sherehe hizo, akisema kwamba mipango imefanywa ili watu wengine 10,000 waweze kuzifuatilia sherehe hizo wakiwa nje ya uwanja, kupitia runinga zitakazowekwa katika uwanja wa Nabii Owuor.

Jana, Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o alisema serikali imefanya mipango ya ziada ili wananchi wafuatilie sherehe hizo kutoka uwanja wa Mowlem.

Kaunti zilizo eneo la Ziwa Victoria zimekuwa katika hali ya tahadhari kutokana na kuongezeka kwa visa vya corona. Kaunti ya Homa Bay iliripoti visa 28 siku ya Jumapili.

Hicho ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kuripotiwa katika kaunti hiyo kwa siku moja. Visa 18 vilikuwa Homa Bay Mjini, sita vikatoka Karachuonyo, Mbita (3) na Ndhiwa kisa kimoja.

Wanafunzi katika shule moja eneo hilo waliagizwa kwenda nyumbani, kuruhusu shughuli ya kupiga dawa, baada ya naibu mwalimu mkuu kufa kutokana na ugonjwa huo.

Katika Kaunti ya Kisii, visa 34 viliripotiwa na kufanya idadi ya jumla ya walioambukizwa kuwa 1,542.

Mkurugenzi wa Afya ya Umma katika kaunti hiyo, Dkt Richard Onkware alisema kufikia sasa Kisii imepima jumla ya watu 10,582.

Waziri wa Afya Kaunti ya Kisumu, Prof Boaz Nyunya, alisema kuongezeka kwa corona eneo hilo kunachangiwa pakubwa na watu kupuuza kanuni, tangu kuondolewa kwa marufuku ya safari za kutoka na kwenda Nairobi.

Ripoti za Rushdie Oudia, Elizabeth Ojina, Ruth Mbula na George Odiwuor

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA