• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Uhuru na Raila wazindua miradi Nairobi na Kajiado

Uhuru na Raila wazindua miradi Nairobi na Kajiado

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS  Uhuru Kenyatta Jumatano alizindua barabara ya umbali wa kilomita 4.2 inayounganisha Kituo cha Makasha cha Nairobi (NICD) na barabara ya pembeni ya kusini (southern by pass) karibu na uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi. 

Akizungumza katika shughuli hiyo, rais, ambaye aliandamana na Waziri Mkuu  wa zamani Raila Odinga, alikariri kujitolea kwa serikali kutatua shida ya msongamano wa magari jijini Nairobi.

“Barabara hii ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukomesha msongamano jijini Nairobi. Itarahisisha mwendo wa magari kwenye barabara ya Mombasa na kusaidia usafirishaji wa mizigo hadi eneo la magharibi mwaka Kenya,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa alipongeza Waziri wa Uchukuzi James Macharia, aliyekuwepo, kwa kuhakikisha barabara hiyo imekamilishwa kwa wakati ufaao na kuambatana na bajeti iliyotengwa.

Naye Odinga alisema amefurahishwa na kuandamana na Rais kushuhudia kufunguliwa kwa barabara hiyo, akisema ustawi wa muundo msingi nchini siku zote umekuwa jambo analolienzi moyoni zaidi.

“Kichochea kikuu cha maendeleo ni ustawi wa miundo msingi nchini. Hii itawawezesha wananchi kufanya biashara kwa urahisi na kujihusisha na shughuli nyinginezo za kuleta mapato,” akasema Bw Odinga ambaye pia ni Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundo msingi.

Baada ya shughuli hiyo Rais Kenyatta, na Bw Odinga, walisafiri pamoja hadi kaunti ya Kajiado ambako alifungua rasmi barabara ya umbali wa kilomita 48 kutoka Ngong kupitia Kiserian hadi Isinya na vilevile barabara ya umbali wa kilomita 43 kutoka Kajiado hadi Imaroro.

Barabara hizo mbili ni za kwanza kuwahi kujengwa kupitia utaratibu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na ile ya kibinafsi kwa gharama ya shilingi Sh 7.8 bilioni.

Rais Kenyatta alisema barabara hizo mbili zitasaidia kufanikisha ustawi wa kiuchumi katika kaunti ya Kajiado na kaunti jirani kando na kupiga jeki sekta ya utalii.

“Kukamilishwa kwa barabara hii kumerahisisha usafirishaji katika eneo hili. Sasa kusafiri hadi Maasai Mara kutoka Loitoktok, haupaswi kupitia Nairobi. Unaweza tu kupitia Imaroro hadi Isinya na kutoka Isinya, Ngong hadi Suswa,” akasema

Mapema, Rais Kenyatta na Odinga walizuru  kituo kipya cha magari ya uchukuzi wa abiria cha Green Park jijini Nairobi ambacho kinajengwa na Idara ya Ustawi wa Jiji la Nairobi (NMS).

Rais ambaye alielekezwa katika ziara hiyo na Mkurugenzi wa NMS anayehusika na Uchukuzi na Ujenzi Mhandisi Michael Ochieng, pia alizindua rasmi hospitali mpya ya daraja la pili katika kituo hicho.

Kituo hicho kipya pia kitakuwa pia na huduma zingine za kisasa ukiwemo mkahawa, duka kubwa la reja reja na kituo cha polisi.

Kituo cha Green Park ni moja kati ya vituo sita vya magari ya uchukuzi wa umma vinavyojengwa na NMS katika sehemu mbali mbali za Nairobi ili kupunguza msongamano katikati mwa jiji.

Vituo vingine viko  kati ya barabara za Desai na Park Road, sehemu za Fig Treem mtaani Ngara, mataa wa Muthurwa na katika makutano ya barabara za Bunyala na Workshop.

You can share this post!

WAPWANI WAPIGWA DAFRAU

Afueni kwa wavuvi kiwanda kikikamilika