RAILA AWASAKA JOHO, MVURYA

Na JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga ameanza mchakato wa kuwashirikisha magavana Hassan Joho na Salim Mvurya kwenye mpango wake wa kuwania urais mwaka ujao.

Hatua hii ikifaulu itakuwa pigo kubwa kwa Gavana wa Kilifi, Amason Kingi, ambaye amekuwa akiongoza juhudi za Wapwani kuwa na chama ama muungano mmoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kauli ya Bw Kingi imekuwa kwamba Wapwani wakizungumza kwa sauti moja watakuwa na usemi mkubwa katika siasa za kitaifa, hatua itakayowasaidia kusukuma ajenda zao kwa nguvu zaidi kuliko wakiunga mkono vyama vya bara.

Duru zimeambia Taifa Leo kuwa Bw Odinga, kwa baraka za Rais Uhuru Kenyatta, ameanza juhudi za kumshawishi Bw Joho kuhusika zaidi katika uongozi wa ODM.

Wakati huo huo Bw Odinga anajitahidi kuhakikisha amemvuta Bw Mvurya upande wake. Gavana huyo wa chama cha Jubilee amekuwa akiegemea mrengo wa Naibu Rais William Ruto.

Ripoti za kuaminika zinaeleza kwamba Bw Odinga anataka Bw Joho kuhusika zaidi katika ODM baada ya kuibuka kuwa Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega huenda akajiunga na mrengo wa Dkt Ruto.

Hatua yake ya kutaka Bw Mvurya kumuunga mkono inatokana na haja ya kuimarisha uungwaji mkono wake eneo la Pwani, hasa baada ya Bw Kingi kuonekana kushikilia ajenda yake ya kubuni muungano wa Wapwani.

Duru za kuaminika zimeeleza Taifa Leo kwamba Bw Odinga ameanza kulenga wanasiasa vijana wakiwemo mabwana Joho, Mvurya na aliyekuwa mbunge wa Funyula, Paul Otuoma.Majuzi Rais Kenyatta alikutana na Bw Joho na Bw Mvurya katika juhudi za kuwashawishi kumuunga mkono Bw Odinga.

NDOTO NA MAONO

Taifa Leo haikufanikiwa kuzungumza na Gavana Mvurya kupata kauli yake kuhusu suala lake kufanya kazi na Bw Odinga.Lakini Bw Joho alikiri kufanya uamuzi wa kumuunga mkono Bw Odinga akisema atahusika zaidi katika handisheki.

“Raila ni babangu kisiasa. Nimekuwa na mazungumzo ya kina naye na nimeshawishika kuwa maono na ndoto zake ambazo zimekosa kutimia kwa miaka mingi wakati huu ziko karibu kufanikiwa kupitia handisheki na BBI,” akasema Bw Joho jana.

“Uhuru pia anaamini ndoto ya Raila. Ndiposa nikaamua kusaidia pale ninaweza. Sitaki kuwa kikwazo cha kutimia kwa maono ya viongozi hao wawili,” akaongeza.

Mbali na kuimarisha ODM, Bw Odinga pia ameanzisha mazungumzo na viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance ambao ni Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetangula (Ford-Kenya) katika juhudi za kuwashawishi kumpa fursa nyingine kwa kumuunga mkono 2022.

Lakini mabwana Musyoka, Mudavadi na Wetangula wamekuwa na mwelekeo tofauti, wakisema walimuunga mkono Bw Odinga mnamo 2013 na 2017 na hivyo sasa ni wakati wake kurudisha mkono kwa kusimama nyuma ya mmoja wao katika uchaguzi wa 2022.

Lakini duru zinaeleza kuwa Rais Kenyatta anajaribu kuwashawishi watatu hao kuhusu haja ya kumuunga mkono Bw Odinga ili kumzima naibu wake Dkt Ruto kuingia Ikulu.

Bw Odinga anaungwa mkono kuwania urais na baadhi ya wakereketwa wa Rais Kenyatta, ambao pia wanataka Bw Moi awe naibu rais.

Wengine ambao Bw Odinga amepanga kushirikisha katika kambi yake ni wabunge Mishi Mboko (Likoni), Zulekha Hassan (Mwakilishi wa Wanawake Kwale), Caleb Amisi (Saboti), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini), Justus Kizito (Shinyalu), Babu Owino (Embakasi Mashariki), George Aladwa (Makadara) na Manson Nyamweya (Mugirango Kusini).

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA