WANASIASA WALIPUA MLIMA

MWANGI MUIRURI NA WANDERI KAMAU

MWELEKEO wa siasa katika ngome ya Rais Uhuru Kenyatta umo taabani kutokana na migawanyiko mingi ambayo imeibuka.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa siasa za Mlima Kenya, Prof Ngugi Njoroge, eneo hilo limejigawa kwa misingi ya kimaeneo, vyama vya kisiasa, uchaguzi wa 2022 na kuhusu msemaji wake.

Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii za Gikuyu, Embu na Meru (Gema), Askofu Lawi Imathiu anasema kuwa eneo hilo limegawanyika vibaya.

“Tumejigawa katika mirengo ya vyama vya kisiasa, kimaeneo, ufuasi wa wawaniaji wa urais na pia katika siasa za kinyumbani,” akasema Askofu Imathiu.

Tayari wanasiasa na wakazi wamegawanyika kati ya wanaomuunga mkono Rais Kenyatta na walio nyuma ya naibu wake William Ruto.

Wanasiasa pia wamegawanyika kimaeneo, ambapo wale wa kaunti za magharibi mwa Mlima Kenya za Nyeri, Murang’a, Kiambu, Nairobi, Laikipia, Kirinyaga na Nyandarua wametofautiana na wenzao wa Embu, Meru na Tharaka Nithi.

Tangu siku za ukoloni, jamii hizo za Agikuyu (Magharibi mwa Mlima Kenya) na zile za Mashariki ambazo ni Ameru, Aembu na Tharaka zimekuwa zikishikilia msimamo mmoja kisiasa.

Jamii za Mashariki zinahisi kuwa sasa ni wakati wao kutoa kiongozi wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya, lakini wenzao wa Magharibi wamepuzilia mbali pendekezo hilo.

Kando na migawanyiko ya siasa za vyama, wazee wa kijamii nao wamegawanyika, utengano mkuu ukijidhihirisha katika kundi la Kikuyu Council of Elders (KCE) mrengo mmoja ukiongozwa na binamuye Rais Kenyatta, Kung’u Muigai huku mrengo mwingine ukiongozwa na mfanyibiashara Peter Munga.

“Eneo hilo limegawanyika kati ya wanaounga mkono Dkt Ruto na walio mrengo wa handisheki kati ya Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga,” asema Prof Njoroge.

“Kimaeneo kuna wanaoshikilia kuwa ukiritimba wa Agikuyu katika kuongoza siasa za eneo hilo unafaa kukomeshwa, na badala yake jamii zingine zichukue hatamu.

“Ndani ya eneo la Magharibi pia kuna mgawanyiko ambapo kunao wanaoshikilia kuwa kaunti Nyeri na Kiambu zimetoa marais, hivyo basi ni zamu ya kaunti za Murang’a, Kirinyaga, Nyandarua na Laikipia kuwa na usemi,” asema.

GEMA WA RIFT VALLEY

Prof Njoroge anaongeza kuwa katika utengano wa msemaji kumezuka mvutano mkuu wa wanaotegea wadhifa huo, ambao wako na vyama vyao vya kisiasa ambavyo wanalenga kutumia kuibuka kidedea kama wasemaji wa kijamii.

Kwa sasa, hafla ya kutawazwa kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kuwa msemaji wa jamii za Mlima Kenya ndiyo imelipua bomu la utengano.

Huku Bw Muigai akiunga mkono hafla hiyo ambayo ilifanyika katika kituo cha utamaduni cha Mukurwe wa Nyagathanga kilichoko Kaunti ya Murang’a, Bw Munga amepinga akitangaza kuwa uhaini ulitendeka.

Mgawanyiko wa maeneo pia umeongezeka baada ya baadhi ya Wakikuyu wanaoishi nje ya eneo hilo kama vile Nakuru na Uasin Gishu kudai kutengwa na wenzao.

“Tumekuwa tukijiuliza kama kwa kweli sisi ni Gema kwa kuwa baada ya kila ushindi wa rais ambaye ni jamii yetu huwa hatupati vyeo katika serikali. Sisi tunafaa kujichukulia kama Gema wa Rift Valley,” akasema Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri.

Aliyekuwa Naibu wa Gavana wa Nyandarua, Waithaka Mwangi aliambia Taifa Leo kuwa wakati umefika wa kila kaunti na kila mwanasiasa aliye na maono ya kuibuka msemaji wa kijamii ajitetee kivyake.

Mgawanyiko mwingine unasababishwa na vyama vingi eneo hilo ambavyo vinatafuta uungwaji mkono wa wakazi.

“Hii migawanyiko yote sio kwa msingi wa kutetea maslahi yetu kama watu wa Mlima Kenya, bali ni ya kusaka makuu kwa baadhi ya viongozi. Itakuwa vyema wananchi waelewe kuwa wao ndio tu wako na suluhu kupitia kufanya maamuzi yao kwa busara,” akasema Askofu Imathiu.

Habari zinazohusiana na hii