• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Walimu hatarini kukosa nyongeza ya mishahara

Walimu hatarini kukosa nyongeza ya mishahara

Na FAITH NYAMAI

WALIMU kote nchini huenda wakakosa nyongeza ya kila mwaka ya mishahara yao pamoja na kupandishwa kwa baadhi ya vyeo baada ya kucheleweshwa kwa majadiliano kuhusu mkataba wa kuboresha malipo yao (CBA) ya 2021-2025.

Hii ni kwa sababu Tume ya Kuwaajiri Walimi (TSC) bado haijatoa ofa kwa miungano ya walimu au kuwaalika kwa mazungumzo ili kuafikiana kuhusu CBA inayopendekezwa.

Hazina Kuu ya kifedha nayo imesema kuwa serikali haina pesa ya kuwaongeza walimu mishahara.

Hapo jana, miungano inayowatetea walimu iliitaka serikali iwaalike ili waafikiane kuhusu mkataba huo wakiapa kwamba lazima wapate nyongeza ya mishahara la sivyo watakumbatia migomo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (Knut) Wilson Sossion alisema kwamba inasikitisha hakuna juhudi zozote ambazo zimefanywa kuhakikisha kwamba maslahi ya walimu yanazingatiwa.

“Kwa sasa mkataba ambao umekuwa ukitumika unaelekea kukamilika. Hii inamaanisha kwamba walimu hawatapata nyongeza ya mishahara wala hawatapandishwa vyeo baada ya Juni,” akasema Bw Sossion.

Mkataba wa sasa wa Sh54 bilioni ulioafikiwa 2017-2021 unatarajiwa kukamilika mnamo Juni 30. Katika mkondo wa mwisho wa utekelezaji wa mkataba huo, walimu 16,152 walipandishwa vyeo kulingana na matamshi ya Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia.

Walimu wengine 1,000 waliofuzu kwa kozi za astashahada (diploma) nao wanatarajiwa kupandishwa vyeo kabla ya Juni kukamilika.

TSC hufuata mkataba ulioafikiwa kabla ya kuwapandisha walimu vyeo au kuwapa nyongeza ya mishahara. Kukosa kuafikia CBA mpya pia kutawaathiri zaidi walimu kwenye kategoria ya C2 ambao hawajapandishwa vyeo tangu mnamo 2015.

Walimu wamekuwa wakilalamika kwamba CBA ya sasa inawapendelea walimu wanaoshikilia vyeo mbalimbali kama walimu wakuu na manaibu wao na kuwaacha walimu wa kawaida bila faida yoyote.

Aidha Bw Sossion alikariri kwamba wametuma CBA kwa TSC ila bado hawajaalikwa kwa mazungumzo yoyote na pia mwajiri huyo hajawapa stakabadhi inayoeleza kuhusu kiasi cha nyongeza ya mshahara ambacho wana uwezo wa kumudu.

Naye mwenyekiti wa Muungano wa Walimu wenye mahitaji maalum James Torome alisema muungano wao tayari umeanza kupokea shinikizo kutoka kwa walimu ambao wanataka kufahamu mengi kuhusu CBA mpya.

“Bado hatujaalikwa na TSC na bado tunasubiri mawasiliano kutoka kwao kuhusu hatima ya suala hili muhimu,” akasema Bw Torome.Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori naye hakuzungumzia suala hilo alipofikiwa na Taifa Leo.

Hata hivyo, afisa mmoja wa TSC ambaye hakutaka atambuliwe alisema kuwa hawawezi kuandaa mazungumzo na miungano ya walimu kuhusu CBA kwa kuwa tume hiyo bado haina makamishna wa kutosha.

TSC kwa sasa ina makamishna wanne ilhali idadi inayohitajika ni tisa. “Majadiliano hayo kuhusu CBA yapo kwenye ajenda yetu. Hata hivyo, kinachosikitisha ni kwamba hazina kuu ya kifedha bado haijatenga bajeti kufadhili utekelezaji wa mkataba huu,” akasema afisa huyo.

Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) nayo imeiandikia TSC ikiomba muda zaidi ili ishauriane na wakuu wa miungano ya walimu kuhusu kusawazisha mishahara.

You can share this post!

Nahitaji miaka 3 kuifahamu vyema idara – Jaji Mkuu...

Rufaa ya BBI kung’oa nanga juma lijalo