• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Muturi aharibu hesabu ya Raila, Ruto Mlimani

Muturi aharibu hesabu ya Raila, Ruto Mlimani

Na WAANDISHI WETU

KUTAWAZWA kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kama Msemaji wa jamii za Mlima Kenya kumevuruga mikakati ya kisiasa ya Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga ambao wote walikuwa wameanza kunyemelea kura za eneo hilo.

Bw Muturi ambaye anaaminika kuwa na baraka za Rais Uhuru Kenyatta, pia amedidimiza zaidi matumaini ya aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth kuwa na usemi mkubwa wa siasa za ukanda wa Mlima Kenya.

Bw Odinga amekuwa akishirikiana na Bw Kenneth kupenya kisiasa katika uchaguzi wa 2022. Kwa upande mwingine, Dkt Ruto amekuwa akitegemea ushawishi wa aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri wa chama cha The Service Party (TSP) ili kujivumisha.

Isitoshe, kutawazwa kwa Bw Muturi kumewagawanya wakazi wa Mlima Kenya huku wale wanaotoka kaunti za jamii za Wagikuyu na jamii za Aembu, Ameru, Tharaka kama Embu, Meru na Tharaka-Nithi wakiuunga mkono hatua hiyo.

Hata hivyo, viongozi wanaotoka Nakuru Kiambu, Murang’a, Nyeri na Kirinyaga ambao ni Wakikuyu nao wamepinga vikali kutawazwa kwa Spika huyo wa Bunge la Kitaifa.

Viongozi wa kaunti za Laikipia na Nyandarua ambazo pia ni sehemu ya Mlima Kenya nao wanaonekana kutojihusisha na siasa hizo.

Wengi sasa wanasubiri kutazama iwapo Bw Muturi atateka siasa za eneo hilo ikizingatiwa ameidhinishwa na viongozi wa mrengo wa Tangatanga ambao pia wanamshabikia Dkt Ruto.

Licha ya kudaiwa kuwa na uungwaji mkono wa Rais, viongozi wa mrengo wa Kieleweke nao wamepinga uongozi wa Bw Muturi katika eneo hilo.

Jana, mbunge wa Tharaka Gitonga Muragura alifichua kwamba, wanalenga kuwasilisha jina la Bw Muturi kama mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto.

“Tutaanza mazungumzo na Dkt Ruto ili kuzungumzia suala la Bw Muturi kuwa mgombeaji mwenza wake. Ni jambo jema likitimia,” akasema mbunge huyo wa Jubilee

Bw Muragura alisema katika eneo la Mlima Kenya Mashariki ni wanasiasa wawili pekee ambao wanapinga kutawazwa kwa Bw Muturi kama Msemaji wa Mlima Kenya na watashauriana nao ili kuwaleta pamoja na wale ambao washakumbatia wazo hilo.

Ripoti za GITONGA MARETE, ALEX NJERU na KENNEDY KIMANTHI

You can share this post!

Kiongozi wa wasiomtambua Mungu hatimaye aonekaniwa na Yesu...

Kafyu kuendelea kwa siku 60 zaidi