• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
RIZIKI: Janga la Covid-19 halizimi shabaha yake kubuni nafasi tele za ajira kwa vijana kupitia biashara ya mikahawa ya kukaanga samaki

RIZIKI: Janga la Covid-19 halizimi shabaha yake kubuni nafasi tele za ajira kwa vijana kupitia biashara ya mikahawa ya kukaanga samaki

Na SAMMY WAWERU

PATRICK Macharia amekuwa katika ufugaji wa samaki kwa muda wa miaka 15 mfululizo.

Aliingilia shughuli hiyo mwaka wa 2006 katika eneo la Ruai, Kaunti ya Nairobi baada ya jaribio la kwanza katika ufugaji tofauti kukosa kuzaa matunda.

Kulingana na masimulizi, ufugaji wa samaki alianza na kidimbwi kimoja, ambapo miezi minane baadaye alivua samaki aliofuga.

“Nilianza na vichengo 500 pekee, watoto wa samaki. Hakuna aliyefariki, miezi minane baadaye,” Macharia anadokeza.

Anasema mapato aliyopokea yalimridhisha, kiasi cha kushawishika kuongeza vidimbwi viwili zaidi, akawa na jumla ya vidimbwi vitatu.

Aidha, vyote alivichimba kwa mikono.

Kufikia sasa, Macharia ana jumla ya vidimbwi 49 eneo la Ruai na Kiamumbi, Kahawa West, Nairobi.

Hufuga samaki aina ya tilapia kwa wingi na kambare. Vilevile, hufuga samaki wa kurembesha, maarufu kama ‘ornamental fish’ kwa Kiingereza.

Ni kutokana na maombi ya wateja, ipatayo miaka mitatu iliyopita Mzee Macharia, alifungua mikahawa ya kuchoma na kukaanga samaki.

“Si wengi wanaojua kuchoma na kukaanga samaki. Wateja walianza kunisihi niwachomee samaki na pia kukaanga ndiposa nikatathmini wazo la kufungua mkahawa,” anaelezea.

Mbali na kukaanga, pia husafu kwa ushumbi wa ugali na mboga za kienyeji na kachumbari.

Ana mikahawa miwili, moja katika eneo la Kiamumbi, Kahawa West na nyingine Ruiru pembezoni mwa Thika Super Highway.

Anaiambia Taifa Leo kuwa biashara ya kukaanga na kuchoma samaki ilikuwa imenoga, hadi Kenya ilipokumbwa na janga la Covid-19.

“Ni biashara ya kipekee na yenye mapato, ila msambao wa virusi vya corona nusra uizime,” asema.

Kulingana na Macharia, alikuwa amenunua mashine za kuongeza samaki thamani, kutengeneza soseji, na kwa sasa ‘zimelala’ kwenye ghala kwa kile anataja kama kuhangaishwa na athari za corona.

Amri ya ama kuingia au kutoka Nairobi na viunga vyake iliyotekelezwa mwaka uliopita, 2020 na pia mwaka huu, Macharia anasema ilichangia kwa kiasi kikubwa biashara yake kurudi nyuma.

Mmiliki wa hoteli ya kuchoma na kukaanga samaki eneo la Kiamumbi, Kahawa West, Kaunti ya Nairobi, Patrick Macharia. Picha/ Sammy Waweru

Alikuwa akipokea oda kutoka nje ya Nairobi, ila marufuku ya kuingia au kutoka eneo hilo yalichangia kupoteza kiwango kikubwa cha wateja.

Ni athari ambazo zilimshurutisha kupunguza idadi ya wafanyakazi. “Ilifika kiwango kupata mishahara ilikuwa kibarua, sikuwa na budi ila kupunguza idadi ya wafanyakazi,” anaelezea.

Kilio chake si tofauti na cha Paul Mwangi, mkulima wa viazimbatata, kabichi, karoti na mimea mingineyo inayochukua muda mfupi kuanza kuvunwa.

Mwangi anasema, marufuku ya kuingia au kutoka Nairobi 2020 yalimsababishia hasara ya maelfu ya kabichi.

“Kabla ya corona, nilikuwa nimepanda vipande 6, 000 vya kabichi. Nilifanikiwa kuuza 300 pekee, na kwa bei ya kutupa. Mazao yaliyosalia niliyalisha mifugo na mengine kuozea shambani,” asema mkulima huyo akikadiria hasara.

Huku taifa likiwa linaendelea kupambana na janga la Covid-19, wataalamu wanahimiza haja ya wakulima kuongeza mazao mbichi ya shambani thamani, ili kukwepa kero la soko wakati wa majanga au mazao yanaposheheni.

“Kwa wakuzaji wa mboga, ninawahimiza wakumbatie mifumo ya kuzikausha, matunda kuunda sharubati na nyanya kutengeneza sauce. Hii ni mifano tu ya kuongeza mazao mbichi thamani, hatua ambayo itayawezesha kudumu mkulima akiendelea kusaka soko,” Steven Mwanzia, mtaalamu wa masuala ya kilimo anashauri.

Wakati wa maadhimisho ya Leba Dei, Mei 1, 2021, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuondoa amri ya ama kuingia au kutoka kaunti tano zilizotajwa kuwa hatari katika maambukizi, na zinazojumuisha Nairobi, Kiambu, Kajiado, Machakos na Nakuru.

Hata ingawa anaendelea kuhimili makali ya corona, Patrick Macharia anasema tangazo hilo ni afueni kwake.

“Shabaha yangu ni kuona biashara ya kuchoma na kukaanga samaki imefufuka ili niweze kubuni nafasi tele za ajira kwa vijana.

“Nina imani ikiimarika na kuboreka, ukiwa na kijana anayetafuta kazi nitaweza kumpa fursa ya kujiendeleza kimaisha,” mjasirimali huyo akasema wakati wa mahojiano.

Alisema kwa sasa lake ni dua tu kwa Mungu, aondolee taifa na ulimwengu hii kasumba ya virusi vya corona na ambayo imelemaza uchumi.

  • Tags

You can share this post!

Thiwasco yaweka mikakati ya uboreshaji wa huduma za maji...

Boresha afya yako kwa kunywa maji fufutende