• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:12 PM
TAHARIRI: Vita vya Knut, TSC havifai wakati huu

TAHARIRI: Vita vya Knut, TSC havifai wakati huu

KITENGO CHA UHARIRI

KUMEIBUKA majibizano tena kati ya Chama cha Kutetea Walimu Nchini (Knut) na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kuhusu nyongeza ya mshahara.

Katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion tayari ameanza kulalamika kwamba walimu wako katika hatari ya kupata marupurupu kuanzia mwezi Julai kwa sababu Mkataba wa Maelewano (CBA) uliotiwa saini mwaka 2017 unakamilika mwisho mwezi huu baada ya miaka tano kutimia. Ni sharti walimu watie saini mkataba mpya ili uweze kuwasaidia kupata nyongeza ya mishahara siku zijazo.

Kulingana na Bw Sossion, tume ya TSC imekataa kualika walimu ili wawe na majadiliano kuhusiana na mkataba mpya utakaoshughulikia nyongeza mpya za walimu. Katibu huyo ameitaka tume hiyo kuelezea itachukua hatua gani kuhusu mishahara na marupurupu ya walimu ikiwa hawatakutana.

Kwa upande wake, maafisa wa Muungano wa Walimu wa Sekondari na Vyuo (KUPPET) wamesema kwamba TSC imewasiliana nao tayari.

Mbali na mgogoro huu, TSC na KNUT imetofautiana kuhusu mpango mpya wa kuajiri wa walimu. Tume hiyo ya walimu imesema haitakuwa ikiwaajiri waliosomea digrii ya kozi ya ualimu (Bachelor of Education) bali wale waliofanya kozi kuhusu elimujamii (Bachelor of Arts) au sayansi ( Bachelor of Science) kwa miaka mitatu na kuhitimu astashahada (diploma) ya ualimu mwaka mmoja.

KNUT imelalamika mno kupinga hatua hii kwa madai kwamba, tume hiyo haikuwashauri kabla ya kufikia uamuzi huo.

Ingawa mabadiliko haya yanaweza kuwa yalichochewa na mageuzi ya mtaala mpya, TSC ilifaa kuhusisha wadau wote kisha kuweka wazi suala hili nzima kwa umma.

Kwa upande mwingine chama cha KNUT kinafaa kuipa tume ya TSC nafasi kufuatilia suala la mkataba mpya wa 2021-2025. Tayari tume hiyo imewasiliana na Tume ya Kukadiria Mishahara Nchini (SRC) ambayo pia imewasilisha mapendekezo kwenye Hazina Kuu ya Kitaifa hili suala lote lishughulikiwe. Itakuwa busara pande zote kusikilizana.

Kwa vyovyote vile, Wakenya hawako tayari kushuhudia migogoro mikali kati ya TSC na Knut kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Sekta ya Elimu kuathirika mno kwa kupoteza muda mwingi bila masomo kutokana na mlipuko wa gonjwa hatari la corona, sawa na sekta zingine, na hakuna lolote linalofaa kukubaliwa kukomesha juhudi na mikakati iliyowekwa kufikia ufanisi huo. Taasisi zote kote nchini zimeanza kutulia na zinafaa kuungwa mkono kwa njia zozote zile.

You can share this post!

WANGARI: Masuala ya hedhi yaangaziwe kwa kina kusaidia...

SHINA LA UHAI: Hedhi salama bado ni changamoto kwa...