Covid-19: Raila atoa wito serikali izindue miradi mingi mashinani raia wapate kazi

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amependekeza kwamba uzinduzi wa miradi ya kazi mashambani ni njia muhimu ya kuokoa walioathirika na janga la Covid-19.

Raila ametoa wito huo wakati akihutubu katika hafla ya maadhimisho ya Madaraka Dei jijini Kisumu, Jumanne.

 

“Kenya kwa sasa ina shida. Tunahitaji mpango kukwamua Wakenya hasa walioathirika zaidi na corona. Miradi ya kazi maeneo ya mashambani izinduliwe, sawa ni ile ya Kazi Mtaani,” akasema kiongozi huyo wa ODM.

Hafla hiyo ya maadhimisho ya miaka 58 tangu Kenya ipate uhuru wa kujitawala, na iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, imekuwa jukwaa la kipekee ambapo Raila amesimulia jinsi alivyougua na kupambana na ugonjwa wa Covid-19.

“Corona ilikuja kunitembelea, ikataka kuniangusha, nikaiuliza wewe ni nani? Nilipigana nayo mpaka nikaishinda,” akasimulia, akisababisha umati kuangua kicheko.

Mwaka 2020, baada ya Kenya kukumbwa na virusi vya corona, serikali ilizindua mpango wa Kazi Mtaani, na ambao umekuwa ukitekelezwa maeneo ya mijini.

Unajumuisha usafi wa mazingira, kama vile kufyeka nyasi kandokando mwa barabaraka, kukusanya taka na kukwamua mitaro ya majitaka, kati ya shughuli nyinginezo za usafi.

Maelfu ya vijana walipata nafasi hiyo ya ajira ya muda.

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA