• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KINA CHA FIKRA: Mafanikio na mazonge tangu tupate madaraka

KINA CHA FIKRA: Mafanikio na mazonge tangu tupate madaraka

Na WALLAH BIN WALLAH

WAKATI unapohesabu mafanikio yako usisahau kuhesabu matatizo yako.

Na unapohesabu matatizo yako, usisahau kuyahesabu mafanikio yako. Hapo ndipo utakapojua jinsi ulivyopambana ukafanikiwa na ulivyoteleza ukalemewa mpaka ukashindwa kufanikiwa ukaambulia hasara na matatizo!

Ukishaupata uwiano huo ndipo uchukue hatua ya kujipongeza kwa kufanikiwa na ujirekebishe ulikolemewa ukazongwa na mazonge! Hivyo ndivyo mambo yalivyo katika maisha ya kweli bila kujidanganya na kudanganyana!

Miaka mingi imepita tangu nchi zetu za Afrika kujipatia madaraka na kujikomboa kutoka katika minyororo ya Wakoloni. Kujitawala kuwa huru ni bora zaidi kuliko utumwa!

Kwa hivyo tunawashukuru sana viongozi wazalendo waliojitoa mhanga kuzikomboa nchi zetu za Afrika! Madhumuni yao yalikuwa ni kutukomboa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kimawazo, kiafya na kielimu ili tupate maendeleo zaidi katika maisha, bashasha, kilimo, uvuvi na ufugaji.

Aidha, walitaka nchi zetu ziboreke katika sekta za viwanda na teknolojia. Lakini je, tumefaulu kikamilifu katika nia na madhumuni yote hayo au la? Endapo hatujafaulu, sharti tujiulize kuna mazonge gani? Kisha tujisahihishe!

Kwa hakika tangu nchi zetu za Afrika zijipatie uhuru zaidi ya miaka hamsini iliyopita mpaka kufikia jana tarehe mosi Juni wakati nchi yetu ilipoadhimisha sherehe ya 58 ya Sikukuu ya Madaraka, hatua nyingi za maendeleo zimepigwa.

Mafanikio mengi yamepatikana nchini Kenya. Barabara nyingi za kisasa zimejengwa. Reli ya kisasa imeunganishwa kutoka Mombasa hadi Naivasha (Suswa).

Bandari nyingi zimekarabatiwa na nyingine zikajengwa upya kama vile bandari ya Lamu na Kisumu ambayo Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta aliizindua akiwa na mgeni wake rasmi, Mheshimiwa Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi.

Kivuko kipya cha waendao kwa miguu cha kuunganisha Mombasa kisiwani na Kwale, kimejengwa! Hayo ni matunda ya uhuru baada ya kujikomboa! Hongera na pongezi sana!

Ndugu wapenzi, tulianza kauli ya leo kwa kusema unapohesabu mafanikio uhesabu mapungufu yako pia! Unaposafiri au unapokimbia kuenda mbele, usiache kutazama nyuma ulikotoka! Licha ya mafanikio na malengo ya kujikomboa, siasa zetu bado ni tete! Tuache siasa za kuraruana badala ya kujengana!

Afya na elimu nchini bado ni ya kubabaisha tu! Madaktari na walimu ni wachache! Dawa nazo adimu hospitalini na kwenye zahanati! Wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara hawatembelewi na wataalam kule vijijini na nyanjani!

Mwisho chunguza uone na usikie lugha ya taifa Kiswahili inavyotumiwa shaghalabaghala mitaani, vijijini, mijini na katika idhaa za vyombo vya habari hapa nchini na watangazaji wanasarakasi! Utashangaa! Lazima tujisahihishe kabla mambo hayajaenda kombo zaidi!

You can share this post!

NASAHA: Kujitolea kukuza vipaji vya wengine kutakupa fursa...

SAUTI YA MKEREKETWA: Pendekezo la TSC kuifanyia mabadiliko...