• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Muller na Hummels wachezea Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu 2018

Muller na Hummels wachezea Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu 2018

Na MASHIRIKA

THOMAS Muller na Mats Hummels walichezeshwa na timu ya taifa ya Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu 2018 katika mechi ya kirafiki iliyokamilika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Denmark mnamo Juni 2, 2021 nchini Austria.

Wanasoka hao wawili pamoja na beki Jerome Boateng waliwahi kufurushwa kambini mwa Ujerumani huku kocha Joachim Loew akipendelea zaidi wachezaji chipukizi.

Ingawa hivyo, Loew anayejiuzulu mnamo Julai 2021, aliwarejesha Muller na Hummels kikosini mwanzoni mwa mwezi wa Mei 2021 kwa ajili ya fainali zijazo za Euro.

Florian Neuhaus aliwaweka Ujerumani kifua mbele katika dakika ya 48 kabla ya Yussuf Poulsen kukamilisha krosi ya Christian Eriksen katika dakika ya 71 na kusawazishia Denmark.

Serge Gnabry alishuhudia kombora lake mwishoni mwa kipindi cha pili likigonga mwamba kabla ya Muller kukosa pia nafasi ya kufunga bao la 39 akivalia jezi za Ujerumani waliotawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.

Mechi dhidi ya Denmark ilikuwa ya 101 kwa Muller kuchezea Ujerumani.

Mbali na Muller na Gnabry, mwanasoka mwingine wa Ujerumani aliyemtatiza pakubwa kipa Kasper Schmeichel wa Denmark ni kiungo mvamizi wa Real Madrid, Toni Kroos.

Denmark wamepoteza mechi mbili pekee tangu Septemba 2018. Wamepangiwa kuvaana na Bosnia kirafiki mnamo Juni 6, siku moja kabla ya Ujerumani kupepetana na Latvia katika gozi jingine la kupimana nguvu.

Denmark wametiwa katika Kundi B kwa pamoja na Ubelgiji, Finland na Urusi kwenye fainali zijazo za Euro. Kwa upande wao, Ujerumani wako katika zizi moja na Hungary, Ufaransa na mabingwa watetezi Ureno.

Kwingineko, fowadi matata wa Borussia Dortmund, Erling Braut Haaland alifunga bao katika dakika za mwisho na kusaidia Norway kucharaza Luxembourg 1-0 kirafiki mnamo Juni 2, 2021. Hakuna kikosi chochote kati ya hivyo vinavyoshiriki kampeni za Euro mwaka huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Phil Foden kuwania mataji mawili kwenye tuzo za PFA ambazo...

Barcelona wajitwalia huduma za beki raia wa Brazil, Emerson