• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Mwanamke afa kwa ‘hofu ya kukamatwa na polisi’ Kilifi

Mwanamke afa kwa ‘hofu ya kukamatwa na polisi’ Kilifi

Na MAUREEN ONGALA

MWANAMKE katika kijiji cha Kwa Mwango, Kaunti ya Kilifi amefariki kwa kile wakazi wametaja kuwa mshtuko uliotokana na msako wa polisi dhidi ya watu ambao hawakuwa wamevaa barakoa mnamo Jumatatu.

Wakazi walisema alikimbizwa katika hospitali ya kibinafsi alipozirai baada ya kushtuka, wakati habari zilipoenea kwamba maafisa wa polisi walikuwa wanakamata watu ambao hawakuwa wamevaa barakoa.

“Alikuwa ameniambia niandamane naye kuchukua pesa alizokuwa akidai wateja wake eneo la Kiwandani. Tulipokuwa tunarudi nyumbani tulikutana na kijana aliyetwambia tuvae barakoa kwa sababu polisi walikuwa wanaelekea upande wetu,” akasema rafiki yake, Bi Nelvina Nzai.

Kulingana na Bi Nzai, kijana huyo alikuwa anawatoroka polisi hao kwa vile hakuwa na barakoa.

“Kitsao alikuwa anang’ang’ana kutoa barakoa yake mkobani lakini hakuwa anaiona. Wakati mmoja alitaka kutoroka lakini nikamwambia atulie na aitafute tu polepole,” akasimulia Bi Nzai.

“Hata alipofanikiwa kuipata alikuwa bado anashindwa kuivaa na akaanza kulalamika kuwa moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi kuliko ilivyo kawaida. Alinishikilia kwa nguvu akisema moyo wake unadunda kwa kasi kisha akaanza kukohoa damu,” akasema.

Alipandishwa pikipiki na kukimbizwa hospitalini na walipokuwa njiani, waliona gari la polisi mbele yao eneo la Kavunjeni likiwa limejaa watu waliokamatwa.

Jamaa yake, Bw Stephen Wanje, alisema marehemu alikuwa anaugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Familia hiyo ililaumu polisi kwa ukatili ambao hufanya raia kuwaogopa hata kama hawana makosa au wakiwa na makosa madogo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, Jonathan Koech, alishauri familia hiyo iwasilishe ripoti rasmi kwa polisi ili uchunguzi ufanywe.

“Ni muhimu upasuaji wa mwili ufanywe kwanza ili kujua chanzo cha kifo. Sisi kama polisi tunataka kufanya kazi yetu kwa kuheshimu haki za binadamu, na kama kuna yeyote aliye na malalamishi kuhusu dhuluma, inafaa apige ripoti,” akasema Bw Koech.

Pia aliwataka raia wafuate sheria kila wakati ikiwemo zinazolenga kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Bi Tecla Katana, ambaye alimlea marehemu, alisema binti yake alikuwa mwenye bidii licha ya kuugua.

“Alikuwa na bidii ya kujitafutia riziki ili kugharimia matibabu yake. Alifariki akijitafutia riziki. Ningali nimeshtuka,” akaomboleza.

Marehemu alikuwa ni mshonaji nguo na muuzaji leso.

Alisema alianza kumlea marehemu pamoja na dadake baada ya wazazi wao kufa alipokuwa na umri wa miaka minne na dadake miaka 10.

You can share this post!

Uhuru atikisa demokrasia

ONYANGO: Serikali iongeze kasi ya utoaji chanjo ya corona