• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Maendeleo yasitolewe kwa marafiki kama peremende

KINYUA BIN KING’ORI: Maendeleo yasitolewe kwa marafiki kama peremende

Na KINYUA BIN KING’ORI

KWA mujibu wa Katiba ya 2010, ni wajibu wa serikali ya kitaifa sawia na za magatuzi kutekeleza miradi inayofaidi wananchi katika maeneo yote nchini bila ubaguzi wa kikabila, kidini, kijamii au kisiasa.

Maendeleo ni haki ya raia, na haifai siasa kupewa nafasi katika kuamua miradi ya kumfaidi mwananchi. Wakenya wote wana haki sawa ya kuonja matunda ya ufanisi wa ushuru wao kupitia miradi inayoanzishwa katika maeneo yao.

Serikali ya kitaifa kwa muda sasa imekuwa ikitekeleza miradi kwa njia ya kupendelea sehemu fulani nchini, na tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2022 nao muda wa kuhudumu wa Rais Uhuru Kenyatta ukiendelea kuyoyoma, tumeshuhudia juhudi ambazo ametia kuhakikisha miradi mikuu imetekelezwa katika eneo la Nyanza ambalo kwa miaka mingi limetengwa na serikali zote tatu.

Japo inatia moyo kuona kwa sasa miradi muhimu ikitekelezwa eneo hilo, inavunja moyo kwani chanzo cha miradi hiyo kupatikana ni handisheki. Yaani iwapo si kiongozi wa upinzani Raila Odinga kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta katika mpango wao wa kuleta maridhiano nchini, basi leo wakazi wa Nyanza wasingefaidi. Je, ina maana kuwa ili eneo fulani lipate maendeleo lazima kigogo wa kisiasa eneo hilo awe rafiki wa kiongozi wa taifa?

Raila Odinga anafaa pia kutuambia ikiwa amebadili itikadi kwamba haiwi lazima kiongozi wa upinzani kuwa na handisheki na Rais ili watu wake wafurahie matunda ya ushuru wao. Huu si mtindo ambao tunafaa kuendelea kuuchangamkia maadamu haiwi fahari kwa maeneo mengine kupata maendeleo huku mengine yakitelekezwa.

Ukosoaji

Namkumbuka Raila, akisuta viongozi wa upinzani hasa magavana na wabunge ambao hapo awali walikuwa wakishirikiana na serikali wakisingizia kutafuta maendeleo. Je, Raila sasa amekubali kunayo matunda ya kushirikiana na serikali hata kiongozi akiwa wa upinzani?

Kila mwaka katika bajeti yetu miradi mingi hutengewa fedha nyingi tu, hivyo si hisani kwa Wakenya kupata maendeleo bali inafaa kufanywa kwa manufaa ya mwananchi mlipa ushuru. Ikiwa ni matibabu bora, miundomsingi bora, viwanda kuundwa au uzalishaji wa chakula kupitia mikakati bora ya wizara ya kilimo ni miradi inayotakiwa kusambazwa katika sehemu zote nchini bila kujali ikiwa wakazi wanaunga au kupinga serikali.

Hakupaswi kuwepo kisingizio chochote kwa eneo lolote kutelekezwa wakati fedha za umma zinapotumiwa katika kupanga mikakati ya miradi ya nchi. Aidha, miradi haifai kukamilishwa kwa malengo ya uchaguzi mkuu wa 2022 bali itekelezwe kwa sababu ni haki ya wananchi walipaushuru na kwa mujibu wa ahadi ambazo viongozi walikuwa wametoa kwa wananchi wakati wa kampeni.

You can share this post!

ONYANGO: Serikali iongeze kasi ya utoaji chanjo ya corona

TAHARIRI: Serikali iangamize madhara ya sigara