• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
TAHARIRI: Serikali iangamize madhara ya sigara

TAHARIRI: Serikali iangamize madhara ya sigara

KITENGO CHA UHARIRI

JUMATATU wiki hii ulimwengu uliadhimisha siku ya kimataifa ya Kukabili Tumbaku.

Ni siku ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO), iliitenga kuhamasisha watu kuhusu athari za tumbaku, hasa uvutaji wa sigara. Mwaka huu, kaulimbiu ni ‘Jitolee Uache Kuvuta’.

WHO imeanzisha kampeni ya mwaka mzima ya kuwasaidia mamilioni ya wavutaji sigara, wanaochukua hatua kamili za kutaka kuacha tabia hiyo.

Kampeni hiyo kwa sasa inahusisha moja kwa moja mataifa 29.

Kenya ni kati ya mataifa ambayo yameathiriwa mno na ugonjwa wa Covid-19. Ugonjwa huo uliwalemea na hata kuwaua watu ambao tayari walikuwa na mapafu mabovu kutokana na moshi wa sigara.

Wizara ya Afya kwa ushirikiano na WHO na shirika la kampeni ya kitaifa ya kupambana na utumizi mbaya wa dawa (Nacada), imeweka mikakati ya kuwasaidia wavutaji kuacha uraibu huo. Imeweka namba ya simu isiyolipishwa 1192.

Takwimu zinaonyesha kwamba wavutaji sigara wana hatari zaidi ya kulemewa na pumzi au hata kufa kutokana na ugonjwa wa corona. Kwa hivyo, kuacha kuvuta ni njia bora zaidi ya kujikinga na ugonjwa huo ambao kwa sasa umeua watu 3,206 kufikia leo.

Ulimwenguni, zaidi ya thuluthi moja (watu bilioni mbili) ni wanaume wanaovuta sigara huku wanawake wakiwa karibu milioni 700.

Hapa Kenya, shirika la African Centre for Corrective and Preventive Action (ACCPA) linaandaa mapendekezo kwa Seneti na Bunge la Kitaifa ili umri wa kuvuta sigara uwe kuanzia miaka 21 badala ya 18.

Hatua hiyo inatokana na kugundulika kuwa kampuni za kutengeneza sigara hulenga vijana wa kati ya miaka 18 na 20. Hiyo inatokana na kuwa mtu anapoanza kuvuta sigara akiwa mdogo si rahisi kuacha.

Humu nchini, uvutaji sigara huchangia vifo 8,000 kila mwaka. Visa vingi vya kansa pia hutokana na uvutaji huo.

Serikali yapaswa kutekeleza jukumu lake la kulinda maisha ya wananchi. Katika baadhi ya miji, kumetengwa maeneo ya kuvutia sigara. Inadhaniwa kuwa kufanya hivyo ni kuwalinda wasiovuta, dhidi ya kuathiriwa.

Sasa ni wakati wa kutumia mbinu ili kuwaondoa wavutaji kutoka kwa minyororo hiyo hatari, hata inapozingatia maslahi ya wakulima wa tumbaku.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Maendeleo yasitolewe kwa...

AKILIMALI: Anajichumia kwa kuunda unga wa mabuyu na mafuta...