• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Arsenal kuagana rasmi na wachezaji tisa mwishoni mwa Juni 2021

Arsenal kuagana rasmi na wachezaji tisa mwishoni mwa Juni 2021

Na MASHIRIKA

ARSENAL wamethibitisha kwamba wataagana rasmi na wanasoka tisa ambao mikataba yao inatamatika mwishoni mwa Juni 2021.

Beki David Luiz na kiungo Martin Odegaard ni miongoni mwa wachezaji hao ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Mikel Arteta kwenye kampeni za msimu mpya wa 2021-22.

Arsenal wanalenga kukifanyia kikosi chao mabadiliko makubwa kadri wanavyopania kujisuka upya baada ya kukosa kufuzu kwa soka ya bara Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.

Wanasoka wengine kwenye orodha ya wale watakaokatiza uhusiano wao na Arsenal mwishoni mwa mwezi huu wa Juni ni kiungo Dani Ceballos na kipa Mat Ryan. Wengine ni chipukizi Levi Laing, Joseph Olowu, Luke Plange na Jason Sraha ambao wameshindwa kuridhisha kwenye akademia.

Luiz, 34, anaondoka Arsenal baada ya kuhudumu Emirates kwa miaka miwili tangu abanduke kambini mwa Chelsea ambao ni watani wakuu wa Arsenal katika eneo la London Kaskazini. Amewajibishwa na Arsenal mara 73 na akawasaidia kutwaa Kombe la FA mnamo 2019-20.

Odegaard, 22, na Ceballos, 24, wanatarajiw akurejea Real Madrid baada ya vipindi vyao vya mikopo kambini mwa Arsenal kukamilika. Kipa Ryan, 29, ambaye ni raia wa Australia, pia anatarajiwa kurejea kambini mwa Brighton baada ya kuchezea Arsenal mara tatu pekee wakati wa kipindi chake cha mkopo ugani Emirates.

Arsenal wameahidi kuagana na idadi kubwa ya wachezaji chini ya Arteta aliyewatema wanasoka Mesut Ozil, Sokratis Papastathopoulos, Shkodran Mustafi na Sead Kolasinac ambaye amerejea Emirates baada ya kipindi chake cha mkopo kambini mwa Schalke 04 nchini Ujerumani kukamilika.

Granit Xhaka, Hector Bellerin, Bernd Leno, Pablo Mari, Alexandre Lacazette na Matteo Guendouzi ni wanasoka wengine wanaotarajiwa kuagana na Arsenal ambao wanavizia wachezaji Raheem Sterling wa Manchester City, Zeki Celik wa Lille na kipa Andre Onana wa Ajax.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Gozi la Community Shield kati ya Manchester City na...

Inter Milan wamteua Inzaghi kuwa kizibo cha kocha Antonio...