• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:55 PM
Argentina na Chile watoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Argentina na Chile watoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022

Na MASHIRIKA

ARGENTINA walipoteza fursa ya kuwapita Brazil kileleni mwa jedwali la vikosi vinavyowania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 kutoka Amerika Kusini.

Hii ni baada ya wanafainali hao wa Kombe la Dunia mnamo 2014 kulazimishiwa sare ya 1-1 na Chile mnamo Alhamisi katika uwanja wa Unico Madre de Ciudades mjini Santiago del Estero, Argentina.

Kabla ya kufunga penalti, nyota Lionel Messi alishuhudia makombora yake mawili yakigonga mwamba wa goli la Chile waliomtegemea pakubwa kipa Claudio Bravo. Chile walisawazishiwa na fowadi wa zamani wa Manchester United na Arsenal, Alexis Sanchez ambaye kwa sasa anachezea Inter Milan ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Sare hiyo iliyosajiliwa na Argentina inawasaza nyuma ya Brazil kwa alama moja zaidi. Brazil ambao watakuwa wenyeji wa fainali za Copa America mwaka huu, ndiyo timu ya pekee ambayo haijapoteza alama yoyote kwenye kampeni hizo za kufuzu kwa fainalo za Kombe la Dunia, na wamepangiwa kuvaana na Ecuador usiku wa Juni 4, 2021.

Chile wanashikilia nafasi ya sita jedwalini huku wakiwa nje ya mduara wa kufuzu kwa alama mbili zaidi baada ya kushinda mechi moja pekee kutokana na tano zilizopita.

Messi ambaye ni nahodha wa Argentina, alisema kwamba anaridhishwa na matokeo waliyosajili dhidi ya Chile licha ya kutotia kapuni alama zote tatu muhimu.

“Kikosi kilicheza vizuri na wachezaji walionana vilivyo licha ya kutocheza pamoja kwa muda mrefu wa takriban miezi sita baada ya mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia kuahirishwa mnamo Machi 2020 kutokana na janga la corona,” akasema mshambuliaji huyo wa Barcelona inayoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Mechi dhidi ya Chile ilikuwa ya kwanza kwa Argentina kusakata tangu jagina wao Diego Maradona aliyewaongoza kuzoa ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 1986 kuaga dunia mnamo Novemba 2020.

Chile walitandaza mchuano huo bila kiungo Arturo Vidal ambaye amelazwa hospitalini baada ya kuugua Covid-19. Bao la Sanchez lilikuwa lake la kwanza dhidi ya Argentina.

Mnamo Juni 8, Argentina watakuwa wageni wa Colombia huku Chile wakiwaalika Bolivia.

Bila ya kujivunia huduma za fowadi Edinson Cavani, Uruguay walilazimishiwa sare tasa na Paraguay na matokeo hayo yanasaza kila mojawapo ya timu hizo na alama saba.

Marcelo Moreno alifungia Bolivia mabao mawili na kusaidia kikosi hicho kujitoa mkiani mwa jedwali baada ya kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Venezuela mjini La Paz. Bao jingine la Bolivia lilifumwa wavuni na Diego Bejarano kabla ya Jhon Chancellor kufutia Venezuela machozi.

Baada ya kupoteza mechi mbili za awali kwa jumla ya mabao 9-1, Colombia walijinyanyua na kuweka hai matumaini yao ya kufunga safari ya kuelekea Qatar mnamo 2022 baada ya kupepeta Peru 3-0. Sawa na Colombia, Peru walikamilisha mchuano huo uliosakatiwa mjini Lima na wachezaji 10 uwanjani baada ya Miguel Trauco kuonyeshwa kadi nyekundu.

Mabao ya Colombia waliokosa maarifa ya Daniel Munoz katika kipindi cha pili, yalifumwa wavuni kupitia Yerry Mina, Mateus Uribe na Luis Diaz.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Katiba Institute yapinga uteuzi wa majaji 34 na kuachwa nje...

Uhuru aadhibu majaji waliozima Reggae ya BBI