• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Polisi watibua mkutano wa wanachama wa UDA Pwani

Polisi watibua mkutano wa wanachama wa UDA Pwani

ANTHONY KITIMO na VALENTINE OBARA

MWENYEKITI wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Johnstone Muthama na Katibu Mkuu Veronica Maina, walilazimika kutoroka Alhamisi polisi walipotibua mkutano wa chama hicho jijini Mombasa.

Mikutano sawa na huo iliyokuwa imepangiwa kufanyika katika maeneo mengine ya nchi kama vile Meru na Nandi pia ilivurugwa na polisi mapema wiki hii.

Wanachama wa UDA sasa wanadai kuwa serikali inawahangaisha ikihofia umaarufu wa chama hicho, hasa baada ya kushinda viti mbalimbali vya kisiasa katika chaguzi ndogo tangu kiliposajiliwa mwaka jana.

“Kama mnadhani UDA imeleta ushindani mkubwa, jambo la busara kwenu ni kuandaa vyama vyenu. Hakuna aliyewakataza kuandaa vyama vyenu ili kuwe na mashindano ya haki,” akasema Bi Maina.

Polisi wa eneo la Nyali jana walikatiza mkutano wa chama hicho kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, wakisema hawakujulishwa mapema kuuhusu, na pia ni kinyume cha sheria zilizopiga marufuku mikutano ya kisiasa wakati wa janga la corona.

Miongoni mwa wanachama wapatao 100 waliohudhuria ni wanaopanga kutafuta tiketi ya UDA kuitumia kuwania viti mbalimbali Pwani kwenye uchaguzi mwaka 2022.

“Polisi watumwe waende kukabiliana na wahalifu wanaokatakata watu mitaani badala ya kutuvamia bila sababu,” akasema mmoja wa wajumbe.

Viongozi wengine wakuu wa chama hicho pia walitoroka wakihofia kukamatwa na polisi.

Baada ya kutimuliwa, polisi waliziba milango ya kuingia katika Hoteli ya Terrace Villa Resort, ambapo mkutano huo ulikuwa umeandaliwa. Maafisa wa UDA walikuwa wameweka usalama mkali langoni ili kuhakikisha ni wanachama walioalikwa pekee ambao wangeingia.

Ujumbe wa mwaliko ambao Taifa Leo iliona ukiwa umetumwa kwa baadhi ya wanachama, ulisema wanachama waliokamilisha malipo ya usajili pekee ndio wangeruhusiwa kuingia.

Bw Ali Mazrui, anayepanga kuwania udiwani katika Wadi ya Jomvu, alilaumu polisi kwa kuvuruga mkutano huo.

“Tulikuwa tumefuata kanuni zote za Wizara ya Afya kuhusu uepushaji wa Covid-19 na hata tukawajulisha polisi. Lakini kabla ya kukamilisha kikao cha kwanza, polisi waliingia kwa mabavu na kutuagiza sote tuondoke,” akasema Bw Mazrui.

Bi Esther Chepng’etich anayepanga kuwania tiketi ya chama hicho kwa kiti cha mwakilishi mwanamke wa Kaunti ya Mombasa, alisema mkutano huo ni miongoni mwa mingine mingi ambayo imepangwa kuwafunza wagombeaji watarajiwa kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa na mikakati ya kampeni za chama.

Chama hicho cha nembo ya wilibaro, kilisema mkutano wa jana ulikuwa umehudhuriwa na wajumbe kutoka kaunti zote za Pwani ambazo ni Mombasa, Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Tana River na Lamu.

Kabla ya polisi kuvamia na kuwatawanya waliokuwepo, Bi Maina alikuwa ametoa wito kwa wajumbe watie bidii ili kusajili idadi kubwa zaidi ya wanachama.

Awali, wabunge wanaoegemea upande wa Dkt Ruto katika eneo la Pwani walikuwa wametangaza kuwa wameweka mipango kabambe ya kukabiliana na umaarufu wa Gavana Hassan Joho. Vile vile, wandani wa Dkt Ruto eneo la Pwani wanatarajiwa kukabiliana na viongozi wanaopanga kuunda chama cha kisiasa wa Wapwani.

Katika mahojiano ya awali, Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali alisisitiza kuwa hakuna muda wa kutosha kutafutia umaarufu chama kipya cha Wapwani kabla Uchaguzi Mkuu ujao.

You can share this post!

Kagwe awaonya Wakenya dhidi ya matapeli wa chanjo ya corona

Ureno kuvaana na Ujerumani kwenye fainali za Euro U-21