• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
WASONGA: Upimaji corona Kisumu uanzishwe mara moja!

WASONGA: Upimaji corona Kisumu uanzishwe mara moja!

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kitaifa inafaa kuanzisha mpango maalum wa kuwapima watu corona, kwa wingi, katika kaunti ya Kisumu kufuatia mapuuza ya kanuni za kuzuia msambao wa ugonjwa huo yaliyoshuhudiwa wakati sherehe za Madaraka Dei Jumanne.

Maelfu ya watu walijazana ndani ya Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Jomo Kenyatta (ambako sherehe hizo zilifanyika) na kando kando mwa barabara za jiji la Kisumu na kuongeza uwezekano wa kusambaa kwa vizuri vya corona. Hii ilikuwa kinyume na maagizo ya Wizara ya Afya, Ikulu ya Rais kwamba ni watu 3,000 wangeruhusiwa kuingia uwanjani humo.

Aidha, wakazi wa Kisumu walikaidi agizo la serikali kuu, na ile kaunti yao, kwamba wafuatilie sherehe hizo wakiwa nyumbani na wasikongamane popote kama hatua ya kudhibiti msambao wa Covid-19.

Lakini mbwembwe, shamrashamra na hamu ya wakazi kushabikia Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga zilichangia wao kujiachilia na hivyo kujiweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Katika hali hiyo, huenda wakazi wengi wa Kisumu, na wageni, waliambukizwa virusi vya corona. Hii ni kwa sababu wengi wao waliokuwa ndani na nje ya uwanja huo hawakuwa wamevalia barakoa, ilivyodhihirika katika picha za vyombo vya habari.

Ama kwa hakika nadiriki kusema kuwa katika msisimko huo, raia, wanasiasa na maafisa wa serikali walikuwa “wakisakata densi” na kifo ikizingatiwa kuwa Kisumu imegeuka kuwa kitovu cha msambao wa aina mpya virusi vya corona inayosababisha maafa nchini India.

Kufikia sasa, zaidi ya watu 20 katika kaunti ya Kisumu wameambukizwa aina hiyo ya virusi vya corona inayojulikana kwa kimombo kama, “Delta variant”, kulingana na Wizara ya Afya. Virusi hivyo, ambavyo ni hatari zaidi zilipatikana kwa mara ya kwanza katika sampuli za wafanyakazi wanne wa kampuni ya Sukari ya Kibos mapema mwezi jana. Wanne hao, ambao ni wa asili ya Kihindi, walikuwa wamewasili nchini kutoka India.

Itakumbukwa kwamba India ilijipata katika hali hatari baada ya serikali kuruhusu mapuuza ya masharti ya corona wakati wa hafla ya kidini ya Kumbh na kampeni kuelekea uchaguzi uliofanyika katika jimbo la Bengal. Matokeo ya hatua hii yaliyokuwa mamilioni ya raia kuambukizwa virusi vinavyosababisha Covid-19 na wengine zaidi ya 200,000 kufariki.

Kwa hivyo, nawalaumu maafisa wa usalama ambao waliwahurusu hata kina yakhe ambao hawakuwa na kadi za mwaliko, kuingia katika uga wa kitaifa wa michezo wa Jomo Kenyatta.

Isitoshe, licha ya shinikizo za waandalizi wa sherehe hizo kwamba watu wasiketi wakikaribiana, waliohudhuria walitagusana kwa ukaribu ilhali baadhi yao walivalia barakoa visivyo.

Kufikia saa nne asubuhi uwanja huo mpya, ambao una uwezo wa kubeba watu 30,000 ulikuwa umejaa. Na ilipotimu wakati wa burudani, viongozi wakiongozwa na Rais Kenyatta waliwaongoza wananchi kusakata densi bila kuchukua tahadhari zozote za kuzuia msambao wa corona.

Rais Kenyatta, Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto walionekana kuchochea msambao wa corona walipohiari kuwahutubia raia waliokuwa wamekongamana kando mwa barabara katika eneo la Kondele.

Wakati mmoja iliwalazimu maafisa wa polisi kufyatua vitoa machozi kuwatawanya halaiki ya wananchi waliojaribu kuziba barabara wakitaka kuhutubiwa na Dkt Ruto, eneo la Kondele.

Hii ndio maana nashauri kwamba upimaji wa corona uendeshwe Kisumu ili kuzuia hali inayoshuhudiwa India kutokea katika kaunti hiyo.

You can share this post!

Ureno kuvaana na Ujerumani kwenye fainali za Euro U-21

MATHEKA: Rais hakufaa kutumia sherehe kutishia mahakama