• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Wito wazee wa nyumba 10 walipwe kusambaza kadi za Huduma Namba

Wito wazee wa nyumba 10 walipwe kusambaza kadi za Huduma Namba

Na MAUREEN ONGALA

WAKAZI wa Mtondia na Kibarani, Kaunti ya Kilifi wameitaka serikali ya kitaifa kuwalipa wazee wa nyumba kumi ili kuwawezesha kutekeleza vilivyo shughuli ya kusambaza kadi za Huduma Namba.

Wazee hao wa nyumba kumi wanazunguka vijijini wakiwapa wananchi kadi zao za Huduma.

Kulingana na wakazi hao, hatua hiyo itawapunguzia mzigo wa kutozwa ada na wazee hao wa nyumba kumi kabla ya kupewa kadi zao za Huduma.

Wakizungumza na Taifa Leo wakazi hao walilalamikia hatua ya wazee wa nyumba kumi kuwatoza ada ilhali kadi hizo za Huduma zinapaswa kupeanwa bila malipo na kusema ilikuwa ni dhuluma.

Kwa upande wake naibu kamishna wa Kilifi Kaskazini Bw Josphat Mutisya alisema wazee wa nyumba kumi hawastahili kuitisha pesa wanapopeana kadi hizo .

Bw Hamisi Ali alisema kuwa wakazi wanatozwa kati ya Sh20 na Sh30.

“Huwezi kumtuma mwananchi kazi kubwa kama hii ambayo inasimamiwa na serikali kuu bila kumwezesha kutekeleza jukumu hilo. Wananchi wamekataa kulipa na kadi za huduma namba bado ziko katika ofisi na wahusika hawajazipata hadi wa leo,”akasema.

Alisema wazee hao hung’ang’ana kuhakikisha kuwa serikali kuu inatimiza malengo yake kwa mwananchi na itakuwa bora iwapo watasaidiwa katika majukumu yao.

Bi Beatrice Mwinga alieleza kuwa wazee wa nyumba kumi hubaki na kadi hizo wakazi wakikosa kuwapa pesa.

You can share this post!

Viongozi wataka kaunti 8 za Mashariki kuungana

Sudan Kusini yakashifiwa kwa ‘kusambaza’ chanjo ya...