• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Nitapigania ugavana tena katika uchaguzi wa 2022 – Korane

Nitapigania ugavana tena katika uchaguzi wa 2022 – Korane

Na FARHIYA HUSSEIN

SIKU chache baada ya Mbunge wa Garissa Aden Duale kuthibitisha kuwa hatowania kiti cha ugavana 2022, sasa Gavana Ali Korane amebaini wazi nia yake ya kupigania kiti hicho.

Gavana huyo ambaye anakaribia kumailisha muhula wake wa kwanza anatoka katika ukoo mkubwa katika Kaunti ya Garissa, yaani Abduwaq.

Gavana huyo amepata msukumo mkubwa kutoka kwa watu wa Fafi na Balambala wanaomtaka apiganie ugavana kwa muhula wa pili.

Maeneo ya Fafi na Balambala yanamilikiwa kiraslimali na jamii ya Rer Harun ambao wanatoka katika ukoo wa Abduwaq.

“Nataka kuwashukuru kwa kuniamini na msaada ambao mmenipa ili nishindane tena kutafuta muhula wa pili licha ya watu wengi kutoamini kazi yangu,” alisema Bw Korane.

Wakiongozwa na mbunge wa zamani wa Fafi, Aden Sugow wanajamii hao walimpongeza gavana huyo wakisema amefanya kazi nzuri ndani ya miaka minne.

“Tumeona rekodi nzuri ya maendeleo katika kipindi cha miaka minne iliyopita na tunaamini gavana anaweza kufanya mengi zaidi ikiwa muda wake utaongezwa 2022. Kama jamii tumejadili na tunataka apiganie tena kiti cha ugavana,” Bw Sugow alisema.

Mwaka wa 2017, Bw Korane ambaye aliungwa mkono na Bw Duale sasa yuko pekee yake, baada ya Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa aliyeondolewa, kujitokeza na kusema kuwa hatamuunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao.

“Nilikuwa nikimuunga mkono kaka yangu Bw Korane mnamo 2017 kwa sababu nilimwamini. Nilijua atawasilisha huduma kwa watu wa Garissa, lakini miaka minne imepita na hiyo haijatokea. Ninaweza kusema Gavana wa zamani Nathif Jama alifanya kazi kubwa hapo awali, ” akasema Bw Duale.

Wawili hao (Korane na Duale) ambao wanatoka katika ukoo mmoja wa Abduwaq walikuwa ndugu wasioweza kutenganishwa katika siasa mnamo 2017, lakini sasa wako katika njia tofauti.

Siasa za Garissa zimekuwa zikiongozwa na koo mbili kuu, jamii ya Abduwaq na Aulian.

Jamii sita kutoka katika ukoo wa Aulian tayari zimejitokeza kumuunga mkono gavana wa hapo awali, Bw Jama kupigania tena muhula wa pili.

Walakini, gavana huyo wa awali bado hajajitokeza wazi kutangaza iwapo atapigania tena ugavana.

Gavana Korane alisema wiki tatu zilizopita alikusanya jamii yote ya Abduwaq na akauliza kila jamii kuwa na mashauriano huru ya umoja juu ya uchaguzi wa mwaka 2022.

You can share this post!

Wales na Albania waambulia sare tasa kwenye mechi ya...

Waislamu Kenya gizani kuhusu kuhudhuria sherehe za hija