• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Tuwei: Sifan ameweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 10,000, lakini mashindano hutofautiana

Tuwei: Sifan ameweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 10,000, lakini mashindano hutofautiana

Na GEOFFREY ANENE

“KILA mashindano hutofautiana.” Hayo ni maoni ya Rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jackson Tuwei baada ya kuulizwa ushindi wa Mholanzi Sifan Hassan wa mbio za mita 10,000 kwa rekodi ya dunia unamaanisha nini kwa Kenya.

Kinadada kutoka Kenya hawajawahi kushinda taji la mbio hizo tangu zijumuishwe kwenye Olimpiki mwaka 1988.Mbio za mita 10,000 za kinadada kwenye Olimpiki 2020 zitaandaliwa Agosti 7 mjini Tokyo, Japan.

Bingwa wa Afrika, Jumuiya ya Madola na Dunia wa mbio za mita 5,000 Hellen Obiri ni mmoja wa wakimbiaji ambao Wakenya wanatarajia atafuzu kuwakilisha taifa. Aliwakilisha Kenya katika Riadha za Dunia 2019 mjini Doha, Qatar akimaliza katika nafasi ya tano.

Sifan alitwaa taji mjini Doha akifuatiwa na Muethiopia Letesenbet Gidey na Mkenya Agnes Jebet katika usanjari huo. Hapo Jumapili, Sifan alitangaza kuwa yeye ni mgombea halisi wa taji hilo baada ya kuweka rekodi mpya ya dunia katika michezo ya FBK Games mjini Hengelo.

Mzawa huyo wa Ethiopia alinyakua taji kwa dakika 29:06.82 baada ya kukamilisha mizunguko hiyo 25. Alivunja rekodi ya Muethiopia Almaz Ayana ya 29:17.45 iliyokuwa imesimama tangu Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016.

Sifan aliamua kuacha wawekaji kasi Mkenya Jackline Rotich na Mholanzi mwenzake Diane van Es ikisalia mizunguko 19. Alizunguka kila mpinzani wake na kumaliza ndani ya muda wa kufuzu kushiriki Olimpiki wa 31:25.00.

Wakenya Irine Kamais (30:37.24), Daisy Cherotich (30:37.31), Joyce Chepkemoi (30:59.01) na Gloria Kite (31:13.04) walifuatana katika nafasi ya pili hadi tano mtawalia.

Medali ambazo Kenya imewahi kushinda katika mbio za mita 10,000 za kinadada kwenye Olimpiki ni fedha kupitia kwa Sally Kipyego (2012) na Vivian Cheruiyot (2016) na nishani ya shaba kutoka kwa Linet Masai (2008) na Cheruiyot (2012).

You can share this post!

Kiungo na nahodha wa Ghana, Andre Ayew, kuagana na Swansea...

Waogeleaji Wakenya Rosafio na Muteti wanatusisimua na...