• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Covid yalipuka Kisumu wiki baada ya ziara ya Uhuru, Raila

Covid yalipuka Kisumu wiki baada ya ziara ya Uhuru, Raila

Na WAANDISHI WETU

RUSHDIE OUDIA, BENSON AMADALA, BENSON AYIENDA, GEORGE ODIWUOR, DERICK LUVEGA, SHABAN MAKOKHA, VITALIS KIMUTAI na IAN BYRON

KAUNTI ya Kisumu imetangaza kanuni mpya za kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19.

Mkurupuko huo umezuka wiki moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhutubia mikutano ya hadhara pamoja na sherehe za Madaraka Dei mjini humo.

Wataalamu wa afya walikuwa wamewaonya wawili hao kuhusu hatari ya mikutano hiyo, hasa ilipogunduliwa kuwa aina mpya ya virusi vya Covid-19 kutoka India ilikuwa imeambukizwa baadhi ya wakazi.Hii sio mara ya kwanza kwa wanasiasa kupuuza hatari ya Covid-19 kwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara, hali inayofuatiwa na maambukizi mengi.

Kabla ya mkurupuko uliozuka mnamo Machi mwaka huu kote nchini, wanasiasa walikuwa wameandaa mikutano ya hadhara katika maeneo mengi.Katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la maambukizi Kisumu, Gavana Anyang Nyong’o aliwahimiza wakazi wakome kuhudhuria ibada katika makanisa, hekalu na misikiti.

Pia alitangaza kufungwa kwa ofisi za kaunti kuanzia jana isipokuwa zinazotoa huduma muhimu.Kati ya makanisa ambayo tayari yamefungwa ni matawi ya Kanisa la Kianglikana ya Alango, Chiga na Riwo. Pia klabu maarufu cha Yatch kimefungwa.

Licha ya maambukizi kuendelea kuongezeka jijini humo, raia wanaonekana kutojali, hali hiyo ikichochea kaunti kuonya kwamba itachukua hatua kali zaidi dhidi ya magari ya uchukuzi wa umma ambayo yanakiuka masharti ya kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Hata hivyo, si Kisumu pekee ambako idadi ya walioambukizwa imekuwa ikipanda kwani hali sawa inashuhudiwa katika kaunti jirani ya Homa Bay, Siaya na Kakamega.Ongezeko hilo limechochea bunge la Kaunti ya Homa Bay ambalo liko likizoni, kuwaita madiwani kwa kikao kujadili mbinu za kukabili maambukizi.

Kati ya masuala madiwani hao wanatarajiwa kujadili ni bohari ya oxsijeni katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Homa Bay.

You can share this post!

Muthama atoa masharti makali kabla ya kuridhiana na Kalonzo

Mvutano wa kuvunja serikali ya Vihiga waendelea