• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Zamu ya Safari Rally kumulikwa baada ya Ogier kushinda nchini Italia mnamo Jumapili

Zamu ya Safari Rally kumulikwa baada ya Ogier kushinda nchini Italia mnamo Jumapili

Na GEOFFREY ANENE

ULIMWENGU mzima unaelekeza sasa macho kwa Mbio za Magari Duniani (WRC) za Safari Rally baada ya duru ya tano kukamilika na ushindi wa Sebastien Ogier nchini Italia mnamo Jumapili.

Mfaransa huyo, ambaye pia alishinda duru ya Monaco na Croatia, ni mmoja wa madereva 58 walio kwenye orodha itakayokuwa nchini Kenya kwa makala ya 69 ya Safari Rally mnamo Juni 24-27.

Ogier aliongoza timu ya Toyota Yaris kufagia nafasi mbili za kwanza katika kisiwa Sardinia. Alinyakua taji la Italia kwa saa 3:19:26.4 akifuatiwa sekunde 46 nyuma na Muingereza na mshindi wa duru ya nne nchini Ureno, Elfyn Evans.

Mbelgiji Thierry Neuville kutoka timu ya Hyundai aliridhika na nafasi ya tatu dakika moja na sekunde tano nukta mbili nyuma ya bingwa mara saba Ogier. Neuville amekamata nafasi ya tatu mara nne msimu huu kutoka duru za Monaco, Finland, Croatia na Italia.

Ogier atafika Kenya akiwa anakalia juu ya jedwali la msimu huu kwa alama 106. Yuko mbele ya Evans kwa alama 11. Neuville na raia wa Estonia Ott Tanak aliyeshinda nchini Finland wamezoa alama 77 na 49, mtawalia. Mjapani Takamoto Katsuta anakamilisha nafasi tano za kwanza kwa alama 48. Tanak na Katsuta pia wanaendesha magari ya aina ya Hyundai.

Safari Rally inarejea kwenye ratiba ya dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002. Hakuna nchi nyingine Afrika iko kwenye ratiba ya WRC. Safari Rally itaandaliwa katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Nakuru ambako sehemu kubwa ya mashindano itafanyika katika mashamba ya eneobunge la Naivasha.

Mabingwa wa duru ya Safari Rally Carl Tundo na Baldev Chager ilipokuwa imeondolewa kwenye WRC na Ian Duncan aliyeshinda duru ya WRC mwaka 1994, ni baadhi ya madereva kutoka Kenya watakaoshiriki makala ya mwaka huu.

You can share this post!

Bandari FC iko tayari kuishinda Equity FC mechi ya nusu...

Mkenya Mudibo achaguliwa naibu rais wa tenisi ya mezani...