• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Phil Foden wa Man-City ndiye mwanasoka mwenye thamani ya juu zaidi barani Ulaya

Phil Foden wa Man-City ndiye mwanasoka mwenye thamani ya juu zaidi barani Ulaya

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

WANASOKA watatu raia wa Uingereza – Phil Foden, Marcus Rashford na Mson Greenwood ndio wachezaji wenye thamani kubwa zaidi miongoni mwa ligi kuu tano za bara Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la utafiti la CIES Football Observatory, Foden wa Manchester City anaongoza jedwali hilo huku thamani yake ikiwa Sh22.87 bilioni. Anafuatwa na wanasoka wawili wa Manchester United – Greenwood (Sh21.39 bilioni) na Rashford (Sh19.12 bilioni).

Kiungo matata wa Man-United na timu ya taifa ya Ureno, Bruno Fernandes anashikilia nafasi ya tano kwa Sh18.5 bilioni. Mason Mount wa Chelsea anafunga orodha ya wanasoka 10-bora kwa thamani ya Sh14.85 bilioni. CIES hutumia vigezo vya umri wa mchezaji, matokeo yake na hali ya soko la uhamisho kuandaa orodha hiyo.

Foden, 21, aliwatambisha Man-City mnamo 2020-21 na akaongoza waajiri wake hao kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) naye akitawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka kwenye tuzo zilizotolewa na Chama cha Wanasoka wa Wataalamu (PFA).

Foden alifunga pia mabao matatu na kuchangia matatu mengine katika safari ya Man-City kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza chini ya kocha Pep Guardiola. Man-City walipigwa 1-0 na Chelsea kwenye fainali hiyo.

Kwa upande wao, Greenwood na Rashford walikuwa nguzo muhimu katika kusaidia Man-United kukamilisha msimu wa 2020-21 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL. Waliongoza pia Man-United kutinga fainali ya Europa League huku wakifunga mabao 12 na 21 mtawalia kwenye mapambano yote.

Ingawa Foden na Rashford walikuwa wawe sehemu ya kikosi cha Uingereza kwenye fainali za Euro, Greenwood alijiondoa kwa sababu ya jeraha la paja.

Fowadi Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund ndiye mwanasoka asiye wa EPL ambaye ni wa thamani kubwa zaidi barani Ulaya. Nyota huyo raia wa Norway alifungia Dortmund jumla ya mabao 41 mnamo 2020-21 na thamani yake ni Sh18.69 bilioni.

Wanasoka wawili wa Barcelona – Frenkie de Jong na Pedri pamoja na Joao Felix wa Atletico Madrid na Alphonso Davies wa Bayern Munich pia wako ndani ya orodha ya 10-bora.

Ederson wa Man-City (Sh7.4 bilioni) ndiye kipa mwenye thamani ya juu zaidi huku Ruben Dias wa Man-City (Sh13.7 bilioni) akijivunia kuwa beki mwenye thamani kubwa zaidi barani Ulaya.

Fernandes, 26, ni mmoja kati ya wachezaji wenye umri wa zaidi ya miaka 25 ambaye thamani yake ni zaidi ya Sh11.2 bilioni. Wengine ni Bernardo Silva, 26, wa Man-City na fowadi matata wa Chelsea, Timo Werner, 25.

 

You can share this post!

Chipu wakamilisha kambi ya mazoezi ya Kombe la Afrika

Gozi la Community Shield kati ya Man-City na Leicester...