• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Moraa atesa mbio za mita 800 nchini Finland kinadada Wakenya wakionyeshwa kivumbi mita 3,000 kuruka viunzi na maji

Moraa atesa mbio za mita 800 nchini Finland kinadada Wakenya wakionyeshwa kivumbi mita 3,000 kuruka viunzi na maji

Na GEOFFREY ANENE

MARY Moraa alikaribia kufikia muda unaohitajika kushiriki mbio za mita 800 kwenye Olimpiki 2020 baada ya kushinda michezo ya Paavo Nurmi mjini Turku nchini Finland, Jumatatu.

Mshindi huyo wa medali ya fedha ya mbio za mita 400 kwenye Riadha za Dunia za Under-18 mwaka 2017, alikamilisha mizunguko hiyo miwili kwa dakika 1:59.95. Muda huu ni wake bora. Hapo awali, muda bora wa Moraa ulikuwa 2:01.12 aliouandikisha katika mchujo wa kuingia mashindano ya kuchagua timu ya Kenya ya Olimpiki mnamo Mei 29 ugani Nyayo.

Mjini Turku, alifuatiwa kwa karibu na Sara Kuivisto (Finland) 2:01.57 na Noelie Yarigo (Benin) 2:01.96 katika nafasi tatu za kwanza. Muda wa kushiriki mbio za mita 800 za kinadada kwenye Olimpiki mjini Tokyo, Japan ni 1:59.50.

Naye mzawa wa Kenya, Winfred Yavi, ambaye ni raia wa Bahrain, alibeba taji la mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa dakika 9:17.55. Alikamisha mbele ya Michelle Finna (Ireland) 9:29.5, Fancy Cherono (Kenya) 9:33.49 na Claire Palou (Ufaransa) 9:34.10. Bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 2,000 za kuruka viunzi na maji za chipukizi Rosefline Chepng’etich kutoka Kenya, hakukamilisha.

Leo, itakuwa zamu ya mshindi wa nishani ya shaba ya mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia 2019 Ferguson Rotich kutafuta ubingwa wa mizunguko miwili ya wanaume. Mkenya mwenzake Cornelius Tuwei pia yuko katika orodha ya washiriki wa mbio za mita 800. Nicholas Bett, Barnabas Kipyego na Wilberforce Kones watawania taji la mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

You can share this post!

KBC kupeperusha Safari Rally, imesaini kandarasi na WRC ya...

Kipa Sergio Romero kati ya wachezaji wanane ambao...