• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Wabunge watisha kuvuruga usomaji bajeti Alhamisi

Wabunge watisha kuvuruga usomaji bajeti Alhamisi

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wametisha kuzuia usomaji wa bajeti bungeni Alhamsi kwa sababu Hazina ya Kitaifa imechelewesha kuwasilisha Sh13.9 bilioni za hazina ya ustawi wa maeneo bunge (CDF).

Wakiongozwa na Mbunge wa Aldai Cornelly Serem wabunge hao walilalamika kwamba Waziri wa Fedha Ukur Yatani alikosa kutimiza hadi yake awali kwamba angetume pesa hizo zote kufikia mwisho wa mwaka huu wa kifedha, Juni 30, 2022.

“Licha ya Waziri Yatani aliahidi kutuma Sh2 bilioni kila wiki miezi ya Mei na Juni, kufikia sasa ni Sh2 bilioni zimetumwa kutoka Sh13.9 bilioni za CDF zilizosalia katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021. Ikiwa pesa hizo hazitakuwa zimetumwa ifikapo Alhamisi, tutavuruga usomaji wa bajeti katika bunge hili,” akasema Bw Serem, akisisitiza hayo “sio vitisho”.

“Sio vizuri kwa bunge hili kujadili mgao wa fedha wa mwaka ujao wa kifedha ilhali fedha za CDF za mwaka huu hazijatolewa zote. Watoto wetu wanataka basari, “ akasisitiza.

Kauli hiyo ya Bw Serem, ambaye mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu CDF inayoongozwa na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi iliungwa na mkono na wabunge wenzake kutoka mirengo yote.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisema maafisa wa Hazina ya Kitaifa wanaohusika wanafaa kuzingatia suala hilo la sivyo “wakabiliwe na hali ngumu Alhamisi.”“Nadhani hao watu kule Hazina ya Kitaifa wamesikia. Huenda wakakabiliwa na mawimbi makali watakapofika hapa,” akasema.

“Unaweza kuwashawishi wabunge hawa kususia kikao hicho au wafanye kile wawezalo kuhakikisha kuwa Waziri anatii ombi lako. Nina uhakika wamekusikia,” Bw Muturi anaongeza.

Hata hivyo, Spika huyo alisema kwa kuwa siku ya mwisho ya mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021 ni Juni 30, huenda maafisa wa Hazina ya Kitaifa wakatuma pesa hizo za CDF kabla ya siku hiyo.

Waziri Yatani anatarajia kusoma makadirio ya mapato na matumizi ya serikali katika kipindi cha mwaka wa kifedha ujao wa 2021/2022 Alhamisi bungeni mwendo wa saa tisa na dakika 15 alasiri. Anatarajiwa kusoma bajeti ya thamani ya Sh3.6 trilioni.

  • Tags

You can share this post!

‘WHO haitaishinikiza Uchina kufichua chanzo cha corona’

Mandazi aina ya ‘kangumu’ yamtia gavana wa...