• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
CHAKIBU: Jivunio la Butula Boys kwa makuzi ya lugha

CHAKIBU: Jivunio la Butula Boys kwa makuzi ya lugha

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Louis Butula Boys, Kaunti ya Busia (CHAKIBU), kiliasisiwa kwa nia ya kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu Kiswahili, kukuza talanta za wanafunzi katika kazi bunilizi, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuboresha matokeo ya KCSE Kiswahili.

CHAKIBU kwa sasa kina mikakati ya kushiriki makongamano mbalimbali ya Kiswahili kwa maazimio ya kuwakutanisha wanafunzi na walimu maarufu wa Kiswahili, wanahabari na waandishi mashuhuri kwa azma ya kuwatia ari ya kuanza kuchapukia lugha hii.

Kuasisiwa kwa chama ni zao la ugunduzi kwamba baadhi ya wanafunzi shuleni Butula Boys walikuwa na udhaifu wa kujieleza kwa ufasaha kupitia mazungumzo na maandishi kila walipotumia lugha ya Kiswahili.

Mbali na hayo, chama hiki vilevile kinawapa wanafunzi fursa na majukwaa mwafaka ya kuendesha midahalo wazi kila wanapozamia haja ya kuangazia masuala mbalimbali yanayofungamana na maendeleo ya jamii kwa jumla pamoja na changamoto zinazowakabili wanafunzi masomoni.

Warsha za aina hii huandaliwa ndani na nje ya shule huku uzingativu zaidi ukielekezwa katika kujadili masuala yanayofungamana na haki za watoto, matatizo yanayowakumba vijana, uongozi katika jamii na nafasi ya vijana katika kuendeleza taifa na utamaduni wa Kiswahili.

CHAKIBU kinanuia pia kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaweza kuzungumza lugha sanifu ya Kiswahili bila ya kuathiriwa na tafsiri za moja kwa moja katika mengi ya maneno.

Wanachama wanafanya juhudi za kutumia misamiati mwafaka ya Kiswahili katika kuelezea dhana zenye utata miongoni mwa watumiaji wa lugha hiyo ndani na nje ya shule. Uzungumzaji na Usikilizaji ni stadi ambazo wanafunzi hawa huzihitaji sana ili kuendesha mijadala yenye mantiki.

Chama hundaa vikao vya mara kwa mara kwa lengo la kutoa nafasi bora kwa wanafunzi kuhamasishana, kukumbushana mambo ambayo yalifundishwa madarasani na kuzamia kwa kina baadhi ya mada ambazo zinawatatiza, hasa katika somo la Kiswahili.

Aidha, wanachama huazimia haja ya kudhihirisha upekee wa vipaji vyao katika kutunga na kughani mashairi, kutegua vitendawili na hata kutamba hadithi chini ya uelekezi wa walimu Edwin Omoding na Isaac Were ambao ni walezi wa chama.

Kupitia CHAKIBU, Kiswahili kwa sasa ni miongoni mwa masomo yanayofanywa vyema zaidi na wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya KCSE katika Shule ya Upili ya Butula Boys.

Hali hii imechangiwa zaidi na kuwapo kwa asasi madhubuti zinazoshirikiana kukitukuza na kukikuza Kiswahili.

You can share this post!

Wakazi kupewa bangi baada kupokea chanjo

Uhuru kuidhinisha Nakuru kuwa jiji la nne Kenya