• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Uhuru kuidhinisha Nakuru kuwa jiji la nne Kenya

Uhuru kuidhinisha Nakuru kuwa jiji la nne Kenya

ERIC MATARA na JOSEPH OPENDA

RAIS Uhuru Kenyatta wiki hii anatarajiwa kuidhinisha rasmi mji wa Nakuru kuwa jiji, baada ya Seneti kupitisha hoja ya kuupandisha hadhi wiki iliyopita.

Maseneta walipitisha hoja hiyo Jumatano wiki iliyopita, kwenye kikao maalum kilichofanyika mjini humo.

Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui ametaja hatua hiyo kama ushindi mkubwa kwa wenyeji, akisema italifungua eneo hilo kwa nafasi nyingi za kukuza uchumi wake.

“Baada ya kuidhinishwa rasmi na Rais, Nakuru itakuwa jiji la nne nchini baada ya Nairobi, Mombasa na Kisumu. Huu ni mwanzo mpya kwa mji huu,” akasema Bw Kinyanjui.

Hata hivyo, Bw Kinyanjui amepuuzilia mbali wasiwasi kuwa hatua hiyo itawafanya wenyeji kuanza kutozwa ushuru, ada za ardhi na kodi za juu.

Badala yake, alisema serikali yake itafanya maamuzi kulingana na mahitaji ya wenyeji. Alisema atakuwa akiwashirikisha wananchi kwenye maamuzi kuhusu masuala muhimu yanayolihusu jiji hilo.

Kupandishwa hadhi kwa mji huu kunamaanisha wenyeji watakuwa wakifurahia miundomsingo bora ya michezo, maji ya kutosha, viwanja vya kisasa, barabara nzuri, huduma bora za uzoaji taka kati ya masuala mengine.

“Hatua hii inamaanisha wenyeji watapata huduma bora. Sababu ni kuwa serikali ya Gavana Lee Kinyanjui inatarajiwa kuimarisha taratibu za mipango ya mji, kulainisha uzoaji taka, kushughulikia suala la uhaba wa nyumba, uwekaji mataa kwenye barabara, kutatua suala la misongamano ya magari kati ya masuala mengine yatakayoufanya mji huu kupata hadhi ya jiji,” asema Bw James Michoma, ambaye ni mtaalamu wa mipango ya jiji.

“Mji huu utafanyiwa mpango mpya ili kusuluhisha tatizo la misongamano, hasa katika eneo la kati (CBD) na barabara kuu. Hivyo, wakazi wataanza kupata huduma bora,” akaongeza.

Tayari, mtaa duni wa Bondeni unatarajiwa kushuhudia mageuzi makubwa baada ya serikali kuanza mradi wa ujenzi wa nyumba za mamilioni ya pesa. Nyumba hizo baadaye zitauziwa wananchi.

Kijumla, serikali inajenga nyumba 605 kwa gharama ya Sh2 bilioni.

Kulingana na Bw David Mwangi, ambaye ndiye mwenyekiti wa Chama cha Utalii cha Nakuru (NTA), hadhi mpya ya mji huo itaboresha na kupanua shughuli zake kiuchumi.

“Tunafurahia sana jambo hilo. Jiji hili halitawavutia wawekezaji pekee, bali litaimarisha pakubwa sekta ya utalii,” akasema Bw Mwangi.

Seneti ilifanya jumla ya vikao saba kabla ya kupitisha hoja hiyo.

You can share this post!

CHAKIBU: Jivunio la Butula Boys kwa makuzi ya lugha

Wanawe Mugabe kortini kupinga mwili ufukuliwe