• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Agizo la Magoha kuhusu karo linapinga ahadi ya serikali

Agizo la Magoha kuhusu karo linapinga ahadi ya serikali

Na BENSON MATHEKA

Agizo la Waziri wa Elimu Profesa George Magoha kwamba walimu wakuu wanafaa kuwatuma nyumbani wanafunzi wazazi wakichelewa kulipa linasikitisha halifai.

Ni amri ambayo haifai wakati huu ambao Wakenya wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Kwa waziri wa elimu anayeelewa kwamba katiba inasema kila mtoto ana haki ya kupata elimu ya msingi, ni makosa kwake kuagiza walimu kuwafukuza wanafunzi shuleni kwa sababu ya wazazi kushindwa au kuchelewa kulipa karo.

Hakuna mzazi anayependa mtoto wake akose masomo akiwa na uwezo wa kulipa karo na kwa hivyo agizo la waziri litaathiri wanafunzi ambao wazazi wao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na janga la corona.

Ni kinaya kwamba serikali inayojipiga kifua kwa kudai imefaulu kuhakikisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule za sekondari inatoa amri inayoweza kufanya maelfu ya wanafunzi kufukuzwa shuleni kwa sababu ya wazazi kushindwa au kuchelewa kulipa karo.

Waziri mwenyewe na maafisa wakuu wa wizara ya elimu amekuwa akisema kwamba hakuna mwanafunzi anayefaa kufukuzwa au kuzuiwa kujiunga na shule ya upili ya umma kwa sababu ya kukosa karo. Amekuwa akisema kwamba serikali imepatia shule pesa za kugharimia masomo na agizo lake linaonyesha ahadi hiyo haitimizwi au serikali imeacha mpango wake wa kufadhili elimu ya shule za upili.

Ikiwa huu ndio ukweli ambao serikali haitaki kusema, itakuwa pigo kwa maelfu ya watoto ambao walikuwa wamepata matumaini ya kuendeleza masomo yao kwa kuwa alitoa tangazo hilo hadharani. Ikizingatiwa kwamba walimu wakuu wamekuwa wakilalamika kuwa wanakabiliwa na wakati mgumu, serikali ikichelewesha kutuma pesa shuleni, agizo la waziri lilinuiwa kuficha utepetevu wa serikali katika kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi.

Kwa hakika, katiba haisemi hili linafaa kuwa jukumu la mzazi alivyoashiria waziri. Agizo hilo, pia liliashiria kuwa kwa kulitekeleza, walimu wakuu waendeleze ubaguzi kwa kulenga wanafunzi ambao wanahisi kwamba wazazi wao wanakataa kulipa karo wakiwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Kwa mtazamo wowote ule, agizo hili ni pigo kwa wanafunzi walioweka matumaini yao kwa ahadi ya serikali kwamba hakuna atakayekosa elimu kwa sababu ya karo

  • Tags

You can share this post!

Ondoa chunusi usoni kwa kutumia maji ya mshubiri(Aloe vera).

NCCK yaonya kuhusu tarehe ya uchaguzi