• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
NCCK yaonya kuhusu tarehe ya uchaguzi

NCCK yaonya kuhusu tarehe ya uchaguzi

Na DAVID MUCHUI

BARAZA la Kitaifa la Makanisa (NCCK), limeonya dhidi ya juhudi zozote za kuahirisha uchaguzi mkuu ujao kikatiba unapasa kufanyika Agosti 9, 2022.

Viongozi wa NCCK eneo la Mashariki, pia walitahadharisha kuhusu walichotaja kama ukosefu wa maandalizi ya uchaguzi huo mkuu ikiwa imebaki miezi 13 ufanyike.Viongozi wa makanisa kutoka Tharaka Nithi, Meru, Isiolo na Marsabit walisema juhudi zote zinafaa kufanywa kuhakikisha kuwa uchaguzi utakuwa wa amani, haki na huru“Kila kitu kinafaa kufanywa kuhakikisha uchaguzi mkuu utafanyika Agosti 9 2022 inavyopasa kikatiba.

Hakuna mtu anayefaa kutumia visingizio kujaribu kubadilisha tarehe ya uchaguzi huo,” alisema mwenyekiti wa tawi la ukanda wa juu wa eneo la Mashariki la NCCK, Padre Samuel Riungu.Kauli ya viongozi hao wa kidini inajiri kufuatia ripoti kwamba wanaounga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI), wanataka kura ya maamuzi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Padre Riungu alisema hayo baada ya kongamano la siku tatu la tawi hilo katika ukumbi wa mikutano wa Gitoro mjini Meru.Bw Riungu alieleza hofu kwamba changamoto zilizopelekea kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017, hazijashughulikiwa huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikikosa makamishna wa kutosha.

“Kongamano hili la kieneo linafahamu kwamba imebaki miezi 13 kabla ya tarehe ya kikatiba ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo, kumekuwa na mapuuza, ya wanaopaswa kuwajibika katika kuweka maandalizi yanayofaa ili nchi iwe tayari kwa uchaguzi mkuu,” alisema.

Pia alilaumu bunge kwa kuchelewa kupitisha sheria za kufanyia mageuzi mfumo wa uchaguzi ikiwemo uteuzi wa vyama vya kisiasa, kura ya maamuzi, kubadilisha sheria ya ufadhili wa kampeni za uchaguzi, wwakilishi wa watu walio na ulemavu na usawa wa kijinsia.

NCCK pia inataka IEBC kuharakisha uteuzi wa makamishna ili ijiandae kwa uchaguzi mkuu.“Tunahimiza afisa ya IEBC na makamishna kuanza kufahamisha Wakenya kila mwezi kuhusu maandalizi inayofanya kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” akasema Padre Riungu.ia,” alisema mwenyekiti huyo wa tawi la NCCK.

Viongozi hao pia wanataka tume ya kitaifa ya Uwiano na Utengamano, IEBC na mashirika mengine yanayohusika kutumia sheria kikamilifu dhidi ya wanaochochea ghasia, kutoa matamshi ya chuki na kulipa magenge kusababisha ghasia.Kuhusu BBI, Padre Riungu alikariri msimamo wa NCCK kwamba mchakato huo uahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa kuwa katiba inagusa na kudhibiti maisha ya Wakenya wote, mchakato wa kuibadilisha ni muhimu, na Wakenya wote wanafaa kupatiwa nafasi ya kutosha na kuelewa ili waweze kushiriki ipaswavyo,” alisema.Viongozi hao wa makanisa walihimiza kushirikishwa kwa vijana kikamilifu katika maendeleo ili kuwalinda kutoka kutumiwa vibaya na wanasiasa wakati wa kampeni.

You can share this post!

Agizo la Magoha kuhusu karo linapinga ahadi ya serikali

Maraga, Mutunga wanguruma