Adai kufungiwa boma hadi abaini ukweli wa kifo cha mtoto wake

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME ambaye mtoto wake alipatikana amefariki ndani ya gari la askofu Mombasa miaka mitatu iliyopita, amefichua alizuiwa kurudi nyumbani na jamaa zake hadi ukweli kuhusu kifo hicho utakapojulikana.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji amefungua uchunguzi kuhusu kifo hicho cha kushangaza cha mtoto wa miaka sita.Katika siku ya mkasa Februari 25, 2018, mtoto huyo, Emmanuel Wasike alihudhuria ibada katika kanisa la Ushindi Baptist, Likoni, kabla kupatikana amekufa saa 12 baadaye akiwa ndani ya gari la Askofu wa kanisa hilo, Bw Joseph Masha.

Babake marehemu, Bw Richard Wanyonyi Wasike jana aliambia mahakama ya Mombasa kwamba jamaa zake wamemkataza kwenda nyumbani Magharibi mwa Kenya hadi atakapokuwa na majibu ya kifo cha mtoto huyo.Bw Wasike, 47, alikuwa shahidi wa kwanza katika uchunguzi huo ambao unasimamiwa na Hakimu Mkuu wa Mombasa Edna Nyaloti.

Aliiambia mahakama kuwa jaribio la familia kupata video wanazoamini zilinaswa na kamera za CCTV ambazo zilikuwa kwenye maegesho ambapo gari lilikuwepo, ziliambulia patupu.

Kulingana na Bw Wasike, swali ambalo halijajibiwa ni kama mtoto huyo aliingia kwa gari mwenyewe au alisukumwa ndani, na aliyefanya hivyo ni nani na alikuwa na nia gani.Familia inaamini kuwa kamera za CCTV zilizowekwa kwenye maegesho, ambayo polisi walidai kuwa haichezi, inaweza kuwasaidia kujibu maswali hayo.

Aliiambia mahakama kuwa siku hiyo, aliwaaga watoto wake watatu walipokuwa wakiondoka kwenda kwa ibada ya watoto kanisani asubuhi.“Walituacha nyumbani tukijiandaa. Ilikuwa ni kawaida wao kututangulia kanisani kwa sababu ibada ya waoto huanza mapema,” akasema Bw Wasike.

Baada ya ibada kukamilika saa kumi jioni, Bw Wasike alisema aliondoka kwenda nyumbani. Watoto wake walibaki nyuma na mama yao.Wakati watoto wengine wawili walifika nyumbani baadaye jioni, marehemu alikosekana. Walianza kumtafuta baada ya kuripoti kisa hicho kwa polisi.

Bw Wasike alisema alipigiwa simu siku iliyofuata na kuambiwa kurudi kanisani kwa sababu mtoto alikuwa amepatikana lakini hakuwa katika hali nzuri.“Nilipata afueni lakini kulikuwa na hisia ambayo si ya kawaida, labda kuashiria kuwa jambo baya,” alisema.