• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Vitengo vinne vikuu kuwakabili polisi watendao maovu

Vitengo vinne vikuu kuwakabili polisi watendao maovu

Na MARY WAMBUI

ASASI nne kuu serikalini sasa zitakuwa zikichunguza mauaji na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaotekelezwa na polisi nchini.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP), Kitengo cha uchunguzi wa masuala ya ndani (IAU), Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) pamoja na Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), zote zitashirikiana kuhakikisha polisi wanaokiuka maadili ya kazi yao wanakabiliwa vikali kisheria.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kuhakikisha raia wanaodhulumiwa na polisi wanapata haki huku wanaotoa ushahidi katika kesi hizo pia wanalindwa au kuhakikishiwa usalama wao.Kwa muda mrefu sasa, uchunguzi ambao umekuwa ukiendelezwa dhidi ya maafisa wanaowaua raia kiholela au kukiuka haki zao, umekabiliwa na changamoto kadhaa kutokana na kugongana kwa majukumu yao.

Aidha, uhasama na ukosefu wa uaminifu kati yao umechangia polisi wanaopatikana na hatia kukwepa mkondo wa sheria.Hili limetokea hasa wakati ambapo visa vya polisi kuwaua raia kiholela au watu kutoweka kwa njia isiyojulikana kuendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali nchini.

Vitengo hivyo vinne ambavyo vinaongozwa na kamati maalum vitamteua afisa mkuu mshirikishi katika afisi zote kwenye kaunti zote nchini ili kurahisisha upokeaji wa ripoti kuhusu visa vingi vya dhuluma za polisi.Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i alisema, wizara hiyo haitavumilia uhalifu au ukiukaji wa haki za raia hata kama utatekelezwa na maafisa wa usalama.

“Kuna ushahidi kwamba polisi wamekuwa wakikiuka maadili ya kazi yao kwa kuwaua raia au kuhusika na visa vya kutoweka kwao. Tuna maadili ya utendakazi na yanafaa yafuatwe na wote kikamilifu,” akasema Dkt Matiang’i katika Chuo cha Mafunzo cha Polisi eneo la Loresho, Nairobi Waziri huyo ambaye amejizolea sifa kama mtumishi wa umma mchapakazi alifichua kwamba, bunduki 14,000 na risasi 400,000 zimetwaliwa kutoka kwa umiliki wa majangali na wahalifu kwa muda wa miaka miwili iliyopita na zinatarajiwa kuteketezwa leo.

“Hawa watu ambao wanaendeleza biashara haramu ya kuchapisha pesa bandia hapa Thika na wengine wanaojificha mitaa ili kuwateka nyara watoto kisha kuitisha fedha, wanaishi miongoni mwetu.“Ni vyema iwapo umma utakuwa macho kuwatambua wahalifu hao. Wengi wao huishi maisha ya kujifanya ili waonekane kama watu tajiri,” akaongeza Dkt Matiang’i.

Msimamizi wa mahakama ya rufaa Daniel Musinga alisema idara ya mahakama inafaa kuboresha ushirikiano wao na vitengo hivyo vya uchunguzi ili kurahisisha utoaji huduma kwa Wakenya.“Kunafaa kuwe na usawazishaji wa majukumu na ushirikiano kati ya idara mbalimbali kwa sababu sote tunawahudumia Wakenya.

Kwa hivyo, tunafaa tuendelee kubadilishana mawazo na mwongozo ili kuboresha huduma zetu,” akasema Bw Musinga.Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Noordin Haji alisema, wanalenga kutathmini hatua zilizopigwa baada ya miaka mitatu katika kukabiliana na uhalifu, uchunguzi na hukumu kwa wanaopatikana na hatia, wawe polisi au raia.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuna uwajibikaji, uwazi, usawa na kurejesha imani ya raia kwenye shughuli zetu zote tunazotekeleza,” akasema Bw Haji.

  • Tags

You can share this post!

Adai kufungiwa boma hadi abaini ukweli wa kifo cha mtoto...

Naibu chifu afumaniwa akishiriki ngono na mwanafunzi