Mbunge ataka fuo na bustani zifunguliwe

Na FARHIYA HUSSEIN

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir amewasilisha hoja bungeni akitaka serikali ifungulie wafanyabiashara bustani ya Mama Ngina na ufuo wa bahari wa Jomo Kenyatta almaarufu Pirates.

Maeneo haya mawili yalifungwa ili kuzuia ueneaji wa virusi vya corona Mombasa na sasa shinikizo inazidi kutolewa kwa serikali kuzingatia maslahi ya mamia ya wakazi waliokuwa wakitegemea maeneo haya kupata riziki.Hata hivyo, endapo serikali itakubali kufungulia wafanyabiashara sehemu hizo, kuna uwezekano wa raia pia kupata mwanya wa kuingia.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, wafanyabiashara hao ni miongoni mwa vivutio vya utalii kwa bidhaa zao na hivyo basi wanapaswa kupewa nafasi ya kufanya biashara zao katika maeneo hayo.“Wafanyabiashara hawa huuza chakula na nguo za kitamaduni. Kwa hivyo ni fursa nzuri ambayo huvutia watalii.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo hayo kwa karibu miaka 30. Kwa sasa hawana pa kuenda,” akasema Bw Nassir.Pia alionya kuwa visa vya uhalifu vinaweza kuongezeka kwa sababu ya ukosefu wa fursa za biashara.Wamiliki wa hoteli Pwani wameunga mkono maoni ya mbunge huyo.

Mkurugenzi Mkuu wa muungano wa wafanyakazi wa hoteli, Bw Sam Ikwaye alisema maeneo hayo yalifanyiwa ukarabati ili kuvutia watalii zaidi na kuwapa nafasi wafanyabiashara wa eneo hilo.“Serikali ilitumia pesa na rasilimali nyingi kuboresha maeneo haya, kwa hivyo yanapaswa kufunguliwa, la sivyo hayatakuwa na maana,’ akasema Bw Ikwaye.

Aliongeza kuwa kufungwa kwa maeneo ya umma kunaweza kuwafukuza watalii wa ndani ya nchi.Hapo awali, wafanyabiashara walikuwa wameitaka serikali ya kaunti na viongozi wa eneo hilo kuingilia kati suala hilo.

“Wafanyabiashara zaidi ya 350 eneo la bustani la Mama Ngina hawana chanzo cha mapato. Tulikuwa tukitegemea kuuza bidhaa zetu hapa, lakini tangu kufungwa hatuna pa kuuzia bidhaa zetu.

Tunashangaa ni kwa nini kaunti zingine zimeruhusiwa kufungua biashara zao wakati sisi tumefungiwa nafasi hizo,” alisema Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mama Ngina, Bw Salim Bawazir.Serikali ilitangaza kuruhusu watu wanaotaka kufanya mazoezi pekee kuingia katika bustani ya Mama Ngina kuanzia Juni 1.