Mshukiwa wa mauaji ya mke aliyekuwa ametoweka anyakwa akijaribu kutorokea nchi jirani ya Tanzania

Na Siago Cece

POLISI katika Kaunti ya Kwale wamemkamata mwanamume ambaye alikuwa ametoweka baada ya kumuua mkewe.

Bw Hammatonn Ismael Karisa amekuwa akikwepa mtego wa polisi kwa miezi kadhaa baada ya kudaiwa kumuua Bi Neema George Karisa mapema mwaka huu, kwa mujibu wa Polisi wa Kuchunguza Uhalifu (DCI).

Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 35 alikamatwa akijaribu kuingia nchi jirani ya Tanzania katika mpaka wa Lungalunga.Taarifa ya wapelelezi inasema kuwa mshukiwa huyo alikamatwa Jumanne baada kuonekana na raia ambaye aliwaarifu polisi.

Bw Karisa anashukiwa kumuua mkewe kutokana na ugomvi wa familia.Wawili hao wanadaiwa kuwa na shida katika ndoa yao iliyosababisha ndoa hiyo kuvunjika. Bi Neema alikuwa amerudi nyumbani kwa wazazi wake eneo la Bamba, Kaunti ya Kilifi.

Bw Karisa alienda kwa wazazi wa marehemu ili kufanya mazungumzo nao kwa nia ya kumaliza mzozo kati yao ili warudiane.“Baada ya mazungumzo, alimshawishi arudi nyumbani pamoja na mtoto wao wa mwaka mmoja. Kumbe huu ulikuwa ni mtego wa kumuua,” taarifa hiyo ilisema.

Baadaye, mwili wa marehemu ulipatikana mtaa wa Jila, Bamba akiwa na majeraha.