Anaoka keki, mikate mtaani Huruma na ndoto yake ni kuwa na matawi kote

Na WINNIE ONYANDO

KUJILINGANISHA na wengine ni adui wa maendeleo. Kila mmoja ana kipaji chake maalum na mtu anapotia bidii na kufanya anachokipenda kwa moyo wake wote, basi hakuna kitakachozuia ufanisi wako.

Hiyo ndiyo kauli ya Daniel Aboyua, mwanamume ambaye amebobea katika sekta ya uokaji mikate, kupika mandazi na kuandaa keki za aina mbalimbali katika mtaa wa Huruma, jijini Nairobi, karibu na kanisa Katoliki la St Daniel Comboni.

Akilimali ilikutana na Daniel, 43, ambaye ana mke na watoto watatu, katika mtaa huo, ambapo alisimulia kuhusu safari ya kuanzisha duka lake la Lexus Bakery mnamo 2018.Anaeleza kuwa baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha nne, alibahatika na kuajiriwa katika duka mmoja la Stage Mart jijini Nakuru kama mhudumu mnamo 2008, kazi aliyoifanya kwa muda wa miezi tisa kabla ya duka hilo kununuliwa na duka kuu la Tuskeys.

Alilazimika kujifunza kuoka mikate na keki baada ya Tuskeys kununua duka alilokuwa akihudumu. Japo hakujua kabisa kuoka mikate na keki, rafiki yake Avistush Vundi alikuwa daraja kwake na kumfunza kila jambo lililohusiana na uokaji mikate na keki.

Baadaye alihamishwa na kuletwa katika mojawapo ya tawi la duka la Tuskeys jijini Nairobi mwaka wa 2009. Hapo alifanya kazi miaka minane kabla duka hilo kufungwa.Anasema kuwa alichoshwa na ajira na hivyo kuungana pamoja na ndugu yake Alfred Okello na kuanzisha biashara ya uokoaji mikate na keki za ladha mbalimbali.

Daniel anakiri kuwa anamshukuru Mungu ambaye amempitisha katika mabonde na milima katika safari yake ya kibiashara na kumfanya kufika alipo sasa.Anaeleza kuwa alipoanzisha biashara, alitengeza biskuti za Sh800 na kuziuza zote. Jambo hilo lilimpa motisha na shauku kuendeleza biashara.

“Kwa kuwa sikuwa nimejenga ukuruba mzuri na wateja, nilianza kwa kutengeza biskuti za Sh5. Nilibahatika na kuziuza zote ila keki zikabaki kidogo. Wateja wangu walikuwa watoto wakati huo. Sikufa moyo ila niliamini kuwa nitafanikiwa nikitia bidii.

Kwa jumla, siku yangu ya kwanza niliuza bidhaa za Sh3,700,” anaeleza Daniel.Kwa kuwa kazi ilikuwa ikimlemea, aliamua kumtafuta msaidizi, alibahatika na kumpata Irine Atieno,35, ambaye hadi sasa amemfunza na kubobea katika uokaji wa keki.

Ili kuoka mikate na keki, kinachohitajika ni mashine spesheli ya uokaji inayotumia nguvu za umeme, mayai, hamira, sukari, ladha mbalimbali za kutengeza keki na siagi.Daniel anasema kuwa kila anachotengeza katika duka lake huchukua muda wa siku nne au saba hivi kabla ya kuharibika.

Anaeleza kuwa anatumia viungo vya kiasili hivyo mikate yake haiwezi kuchukua muda wa wiki moja kaba ya kuharibika.“Kinachonipa motisha ni kuwa kabla ya siku mbili huwa tayari nimeuza karibu kila kitu. Bidhaa zangu hazirundiki dukani kwa kuwa wateja wameongezeka.

Wateja wangu si watoto pekee bali hata watu wazima kutoka mitaa mingine,” anasema.Kufikia sasa, wateja wa Daniel hutoka sehemu mbalimbali jijini Nairobi. Wengine hutoka katika mtaa wa Umoja, Buruburu, na hata Kariobangi kutokana na utamu wa bidhaa zake.

Anasema kuwa si lazima tu ategemee wateja kutoka mtaa wa Huruma.Anakiri kuwa hawezi kukosa Sh3,000 au Sh4,000 mfukoni kila siku ambazo hutenga sehemu na kuweka akiba itakayomsaidia kujiendelea kibiashara.Vile vile, anapanga kununua jenereta ili iweze kumsaidia hasa wakati stima hupotea akiwa anaoka keki zake, hatua ambayo itampunguzia hasara anayokumbana nayo wakati mwingine.