• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Mwili watoweka kaburini

Mwili watoweka kaburini

Na MAUREEN ONGALA

POLISI wa eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo mwili wa nyanya wa miaka 77 ulitoweka kaburini mwake katika kijiji cha Birikani, Mazeras.

Fatuma Mwero alikuwa amezikwa Februari 27 mwaka huu, na mwili wake ulifukuliwa na watu wasiojulikana Jumatatu usiku.

Mzee Juma Lwambi, mume wa marehemu, alisema walishtuka sana walipoambiwa na mwanakijiji kuwa kaburi lilikuwa wazi na mwili haukuwepo.

Walikuwa wameoana kwa miaka 65, tangu mwaka wa 1966 wakabarikiwa watoto saba lakini wanne walifariki.

“Sijui wamepeleka wapi mwili wa mke wangu. Pengine wameamua kwenda kuutupa baharini au kuuchoma,” akasikitika Mzee Lwambi.Alishuku kuwa kisa hicho kimesababishwa na mzozo wa ardhi kati ya familia yake na mwekezaji anayedai umiliki.

Kulingana naye, waliishi katika ardhi hiyo ambayo walipokea kutoka kwa mzungu aliyerudi kwao miaka ya sitini baada ya kupata idhini ya mahakama.Walikuwa wameanza kuhalalisha umiliki wa ardhi mwaka wa 2012, lakini anadai kuna mawakili walioingilia na kuanza kuuzia wawekezaji ardhi hizo.

Cha kushangaza ni kuwa, mwekezaji aliyekuwa akizozania ardhi hiyo ya ekari 15 alifariki siku mbili baada ya mazishi ya Fatuma.

“Ninashuku mwana wake ndiye alihusika kufukua mwili wa mke wangu. Mke wangu pekee ndiye mtu mzima aliyezikwa hapo. Wengine ni watoto watatu ambao makaburi yao hayaonekani,” akadai Mzee Lwambi.

Alisema family ayake haitafanya matambiko yoyote bali watafunika kaburi hadi wakati mwili utapatikana.Chifu wa lokesheni ya Rabai, bw Anthony Jao, alisema mwili ulichukuliwa kwa jeneza lake, na kukaachwa msalaba, maua na kitambaa cheupe kilichokuwa kimefunika jeneza.

Picha/Hisani
KABURI ambapo mwili wa marehemu Fatuma Mwero, 72, ulitoweka katika kijiji cha Birikani, Kaunti Ndogo ya Rabai. Jamaa wanashuku mwili huo uliibiwa na watu wasiojulikana Jumatatu usiku.

Mabati yaliyokuwa yametumiwa kufunika kaburi pia yalibebwa.“Tumeshtuka sana. Hatujawahi kuona visa aina hii katika eneo letu ambapo miili ya wafu inaibiwa kaburini,” akasema.

Akithibitisha kisa hicho cha kushangaza, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Rabai, Bw Fredrick Abuga alisema juhudi za maafisa wa polisi kutafuta mwili huo zilikuwa hazijafua dafu.

Kulingana naye, mwekezaji anayezozania ardhi hiyo alikuwa amepeana familia ya marehemu agizo la mahakama kuzuia mazishi yake.

“Familia ya marehemu haikutii agizo la mahakama na wakamzika katika ardhi hiyo. Anayedai kuwa mmiliki alirudi mahakamani baada ya hapo lakini hatujapokea mawasiliano yoyote tangu wakati huo,” akasema.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Anaoka keki, mikate mtaani Huruma na ndoto yake ni kuwa na...

Wakulima wahimizwa kukumbatia kilimo cha maparachichi ya...