• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
Barabara zafungwa jijini bajeti ikisomwa

Barabara zafungwa jijini bajeti ikisomwa

Na CHARLES WASONGA

KAMANDA  Polisi eneo la Nairobi James Kianda ametangaza kuwa barabara nne Alhamisi,Juni 10, 2021 zitafungwa kwa muda kutoa nafasi kwa Waziri wa Fedha Ukur Yatani kufika bungeni kuwasilisha bajeti.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Bw Kianda alisema barabara za Parliament Road, Taifa Road, Harambee Avenue na City Hall Way zitafungwa, kwa matumizi ya magari ya kawaida,  kuanzia saa saba mchana hadi saa kumi na moja na nusu jioni.

“Ili kutoa nafasi kwa usafiri wa Waziri wa Fedha na maafisa wa Hazina ya Kitaifa kuelekea bungeni kwa ajili ya usomaji wa bajeti barabara hizi nne zinazokaribia majengo ya bunge. Zitafungwa kutoa nafasi kwa Waziri, maafisa wa Hazina ya Kitaifa, wabunge na wageni wengine watakaoelekea bungeni.

Wenye magari wanashauriwa kutumia barabara mbadala,” Bw Kianda akaeleza kwenye taarifa hiyo.Waziri Yatani anatarajiwa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Mwaka wa Kifedha wa 2021/2022 kwenye kikao cha pamoja cha wabunge na maseneta katika majengo ya bunge mwendo wa saa 3.15 alasiri.

Katika bajeti ya kima cha Sh3.6 trilioni, Serikali Kuu imetengewa Sh1.9 trilioni, Asasi ya Bunge imetengewa Sh37 bilioni, Idara ya Mahakama imetengewa Sh17 bilioni huku Serikali za Kaunti zikitengewa Sh370 bilioni. Fedha hizo zitaaanza kutumika kuanzia Julai 1, 2021, mwanzo mwa mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Ili kufadhili bajeti hii, Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru (KRA) imetwikwa wajibu wa kukusanya mapato ya kima cha Sh2 trilion.Serikali inatarajia kujaza pengo ya Sh926 bilioni katika bajeti hiyo kwa kukopa Sh661 bilioni kutoka mashirika ya fedha humu nchini na Sh291 bilioni kutoka nje.

Serikali pia inatarajia kupokea Sh62 bilioni kama ruzuku kutoka mashirika ya kimaendeleo ulimwenguni.Serikali inatarajia kukusanya Sh11.6 bilioni kutokana na ongezeko la ushuru unaotozwa bidhaa za kuingizwa nchini hadi kiwango cha asilimia 15. Bei ya pikipiki za bodaboda pia zinatarajiwa kupanda kutokana kupanda kwa ushuru unaotozwa sawa na bei ya bidhaa za kimsingi kama vile mkate ambayo sasa itatozwa ushuru wa thama, maarufu kama VAT.

  • Tags

You can share this post!

Celtic waajiri kocha Ange Postecoglou kujaza pengo la Neil...

Maseneta washangaa waziri wa Nairobi akifika mbele yake...