Maseneta washangaa waziri wa Nairobi akifika mbele yake akionekana ndani ya bafu

Na CHARLES WASONGA

WANACHAMA wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya Jumatano asubuhi walipigwa na butwaa wakati ambapo Waziri mmoja wa Serikali ya kaunti ya Nairobi alipohudhuria kikao cha kamati hiyo kupitia mtandao wa Zoom akiwa “ndani ya bafu”.

Waziri huyo Bw Mitan Majevdia ambaye alikuwa ameingia katika mkutano huo huku akionekana amevalia mavazi ya bafu.Serikali ya kaunti ya Nairobi na Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) zilikuwa zimealikwa kufika mbele ya kama hiyo kujibu maswali kuhusu matumizi wa fedha za kupambana na janga la Covid-19, kama yalivyoibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Huku akielezea masikitiko yake kuhusu tabia ya Bw Majevdia, Seneta wa Wajir Abdullahi Ali alisema waziri huyo wa afya katika kaunti ya Nairobi alidharau kamati hiyo.“Ni jambo la kusikitisha kwamba afisa wa kaunti anadiriki kufika mbele ya kamati hii ya seneti bila kuvalia vizuri kando na kutokuwa na majibu ya kutosha,” akasema.

Waziri Majevdia pia alionekana kuwa hakuna tayari kujibu maswali yaliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu kwa sababu hakuwa amewasilisha stakabadhi zenye majibu.“Sina majibu wakati huu. Stakabadhi zenye majibu ya maswali yaliyoibuliwa na Mkaguzi wa Hesabu ziko na Katibu wa Kaunti na Naibu Gavana,” akasema.

Lakini Katibu wa Kaunti Justus Musumba alisema hawakuwa wamepokea mwaliko rasmi kufika mbele ya Kamati hiyo ya afya. Kauli hiyo, hata hivyo, ilipingwa na makarani wa kamati hiyo ya seneti inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito.

Baadaye Dkt Mbito aliamuru kwamba Bw Majevdia aondoke katika mkutano huo.“Huyu waziri anaonekana mlevi, yuko ndani ya bafu na hajavaa inavyostahiki. Fedha za Covid-19 ni muhimu na anafaa kuchukulia suala hilo kwa uzito,” akaeleza.