Beki Okumu avutia klabu bingwa barani Ulaya

NA JOHN ASHIHUNDU

Lorient imezidisha juhudi za kuwania saini ya Joseph Okumu wa Harambee Stars anayechezea klabu ya Elfsborg nchini Sweden na huenda beki huyo wa katikati akaanza kusakata nchini Ufaransa kuanzia msimu ujao.

Mbali na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ambayo tayari imeweka mezani zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya kumnasa Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 24, beki huyo wa zamani wa Chemelil Sugar amevutia timu kubwa nchini Scotland na Ubelgiji.

Klabu ya Reims iliyomaliza katika nafasi ya 14 nchini Ufaransa na Rangers ya Scotland pia zimonyesha nia ya kumtaka staa huyo.Rangers inayoandaliwa na aliyekuwa nahodha wa Liverpool Steven Gerrard ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya, msimu ujao.

Celtic inayoshiriki ligi kuu ya Scotland pamoja na Ghent ya Ubelgiji pia zinapigania saini ya staa huyo, lakini ofa zao ni ndogo ikilinganishwa na timu ofa inayotolewa na timu za Ufaransa.Aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars, Musa Otieno ni miongoni mwa waliomtunukia sifa mwanasoka huyoi kutoka na umakini wake anapokuwa uwanjani.

“Nilimtambua alipokuwa akiichezea Chemelil miaka mitano iliyopita na nikawashauri Free State Stars ya Afrika Kusini wamesajili kabla ya kuitwa katika kikosi cha Harambee Stars,” alisema Otieno ambaye aliichezea Santos ya Afrika Kusini kwa miaka mingi.

“Ni kijana aliye na nidhamu ya hali ya juu, mwenye bidii, vitu ambavyo ni muhimu kwa mchezaji yeyote anayetaka kupiga hatua michezoni. Nina hakika atafaulu na kucheza kufikia viwango vya akina Michael Olunga, Ayub Timbe n ahata Eric ‘Marcelo’ Ouma ambao pia ni tegemeo katika kikosi cha Harambee Stars,” aliongeza.