Bajeti 2021/2022: NMS yakumbukwa

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kustawisha Jiji la Nairobi (NMS) limepata mgao wa zaidi ya Sh100 milioni ili kuendeleza majukumu yake.

NMS ilianzishwa mapema 2020 na Rais Uhuru Kenyatta ili kuimarisha utoaji huduma jijini Nairobi na viunga vyake.Baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi, yalipokezwa NMS.

Aidha, shirika hilo linaongozwa na Jenerali Mohamed Badi“Mbali na mgao wa Sh100 katika Makadirio ya Bajeti Mwaka wa Fedha 2021/2022, NMS pia itapata Sh102 milioni zaidi kujenga madaraja ya watu kuvukia katika barabara mbalimbali Nairobi,” akasema Bw Ukuru Yattani, Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa wakati akisoma bajeti ya matumizi ya fedha za serikali ya kitaifa.

Rais Kenyatta amekuwa akipigia upatu na kupongeza utendakazi wa NMS.Shirika hilo limetajwa kusaidia kuangazia uhaba wa maji Nairobi, kupitia uchimbaji wa mashimo ya maji, uboreshaji wa barabara katikati mwa jiji, kati ya miradi mingineyo ya maendeleo.