Bajeti 2021/2022: Biashara ndogondogo na za wastani, Juakali zatengewa mgao wa Sh10 bilioni

Na SAMMY WAWERU

SEKTA ya biashara ndogondogo na zile za kadri maarufu kama SMEs zimetengewa kima cha Sh10 bilioni katika Makadirio ya Bajeti mwaka wa Fedha 2021/2022.

Akisoma makaridirio hayo ya matumizi ya fedha za serikali kuu, Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa, Bw Ukur Yattani alisema mgao huo utasaidia kukwamua sekta hiyo na ambayo ni kati ya zilizoathirika kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona nchini.

“Mgao huo ni asilimia 0.1 ya fedha jumla za makadirio ya bajeti,” akasema Waziri Yattani, akihutubia taifa bungeni.Makadirio ya Bajeti mwaka wa Fedha 2021/2022, yametengewa kima cha Sh3.66 trilioni.

Sekta ya SMEs na Juakali inakadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini.Licha ya serikali kutangaza kuitengea mgao wa fedha, miaka nenda miaka rudi, wafanyabiashara husika wamekuwa wakilalamikia kutopata mgao huo.