• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Askari Jela taabani

Askari Jela taabani

By RICHARD MUNGUTI

ASKARI jela watatu walioshtakiwa jana kwa kupokea zaidi ya Sh48 milioni katika sakata ya kutafutia watu kazi waliachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni.

Watatu hao Sajini Grace Nyamahogo almaarufu kwa jina Nasra alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Kennedy Cheruiyot, pamoja na Jackson Mureithi Manyara na Zachary Kimathi Cosma.

Sjni Nyamahogo alishtakiwa pamoja na binamuye Bw Masiaga Sylvester David na Bw Peter Ngere Githu.Washtakiwa hao walikanusha mashtaka 72 ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu kutoka kwa watu wanaotafuta ajira.

Bw Cheruiyot alielezwa na afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Nicholas ole Sena kwamba washtakiwa walikuwa wakiwaeleza wahasiriwa kwamba watawatafutia kazi katika idara na mashirika ya Serikali.

“Washtakiwa waliwaeleza walalamishi watawatafutia kazi katika Huduma ya Kitaifa ya Polisai (NPS), Idara ya Polisi wa Utawala , Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA), mamalaka ya kupambana na uingizaji nchini bidhaa ghushi (ACA),” mahakama ilifahamishwa.

Mashirika mengine walalamishi waliyoelezwa watapewa ajira ni tume ya kitaifa ya kusimamia masuala ya ardhi (NLC) na mamlaka ya kitaifa ya ujenzi wa barabara (Kenha).Sjni Nyamahogo na Masiaga walikabiliwa na mashtaka zaidi ya 20 ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu.

Walishtakiwa kupokea Sh4.6milioni kutoka kwa Bi Margaret Mbula wakidai watatafutia kazi watu 14 wake katika mashirika mbali mbali ya serikali.Washtakiwa walishtakiwa kupokea mamilioni hayo kati ya Septemba 1 2020 na Machi 31 2021 katika makazi ya idara ya magereza Viwandani.

Askari jela hao waliowakilishwa na mawakili Victor Olao na Jason Maranga walikanusha mashtaka yote 72 kisha wakaomba waachiliwe kwa dhamana.Mabw Olao na Maranga waliiomba mahakama isishawishiwe na idadi ya mashtaka na kiwango cha pesa kinachodaiwa kilipokewa washtakiwa katika kashfa hiyo ya ajira.

Bw Maranga anayemwakilisha Sjni Nyamahogo na binamuye Masiaga alisema dhamana haipasi kuwa kiwango cha juu kiasi kwamba mshukiwa hawezi kukipata.“Kiwango cha juu cha dhamana ni njia moja ya kuwanyima washtakiwa dhamana,” alisema Bw Maranga.

Bw Maranga alifichua kwamba Masiaga ni binamuye Sjni Nyamahoga na walikuwa wakiishi pamoja katika nyumba za askari jela gereza la eneo la Viwandani.“Masiaga hajaajiriwa.Angali anatafuta kazi na endapo atapewa dhamana ya kiwango cha juu basi utakuwa ni mzigo tu kwa Sjni Nyamahogo atakayemlipia,” Bw Maranga.

Bw Olao alisema askari jela huyo alifanyiwa upasuaji mapema mwaka huu na bado “hajapona.”Wakili huyo aliomba mshtakiwa huyo asizuiliwe katika gereza la Langata anakohudumu kwa vile “atatangamana na askari jela wenzake na kufungiwa pamoja na mahabusu aliokuwa akiwatunza na kuwalinda kila siku.”

Mahakama iliombwa iamuru apelekwe gereza la Thika.Mawakili hao waliomba mshtakiwa apelekwe hospitali.Naye Bw Manyara mwenye umri wa miaka 52 alieleza mahakama anaugua ugonjwa wa kisukari na “tangu akamatwe na kuzuiliwa hajapokea matibabu kama alivyoagizwa na daktari wake.”

Lakini kiongozi wa mashtaka alieleza mahakama hapingi washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana ila aliomba korti itilie maanani kiwango cha pesa wanachodaiwa walipokea.Pia hakimu aliombwa azingatie adhabu kali watakayopata washtakiwa kesi dhidi yao ikithibitishwa.

Bw Cheruiyot aliwaachilia Sajini Nyamahoga na binamuye Masiaga kwa dhamana ya Sh2milioni pesa tasilimu kila mmoja.Washtakiwa wale wengine waliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu kila mmoja.Kesi hiyo itatajwa tena Juni 21 kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Bajeti 2021/2022: Michezo ya kamari kutozwa ushuru wa...

Tamu ya penzi ni vitendo